27.6 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wananchi Dar wafurahia punguzo bei ya sukari

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Baadhi ya wafanyabiashara wa rejareja na jumla jijini Dar es Salaam wameendelea kuuza sukari kwa bei elekezi iliyotangazwa na Serikali kutokana na kuimarika kwa upatikanaji wa bidhaa hiyo.

Tani zaidi ya 100,000 ziliwasili nchini tangu mwezi uliopita kukabili changamoto iliyokuwa imejitokeza ya uhaba wa sukari na kusababisha bei kupanda katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Mmoja wa wananchi Bashir Mwanyero ambaye alikutwa akinunua sukari katika duka la Mfanyabiashara Komail Ridhiwan aliyepo Mtaa wa Mtendeni Kisutu, amesema amelazimika kufuata mahali hapo kwa sababu mtaani bado inauzwa kwa zaidi ya Sh 3,200.

Mfanyabiashara Komail Ridhiwan akimuuzia sukari Bashir Mwanyero kwa bei elekezi ya Serikali ya Sh 2,600 kwa kilo.

“Nimenunua kilo mbili, kilo moja nimeuziwa kwa Sh 2,600 nimeshangaa kwa sababu mtaani ninakoishi bei bado haijashuka.

“Tunaomba viongozi wafuatilie utekelezaji wa bei elekezi kwa vitendo kwa sababu wako baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiuza juu ya bei elekezi ya Serikali,” amesema Mwanyero.

Mwananchi mwingine mkazi wa Temeke, Asia Mbawala, amesema; “Nimefurahia kushushwa kwa bei ya sukari kwa sababu mtaani ninakoishi kilo moja inauzwa Sh 4,000 kwa kilo ndio maana nimekuja kununua huku kwa ajili ya futari ya wanangu. Wafanyabiashara wengine wapunguze bei kwa sababu sukari ni kiungo kikubwa kwenye futari.

Naye Mfanyabiashara Komail Ridhiwan, amesema idadi ya wateja wanaonunua sukari imeongezeka baada ya kuuza kwa bei elekezi ya Serikali.

Amesema amekuwa akiuza Sh 2,600 kwa kilo na bado amekuwa akipata faida na kuwasihi wafanyabiashara wengine kupunguza bei ya bidhaa hiyo ili kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wa kipato cha chini.

“Wafanyabiashara tuwe wazalendo ni afadhali upate faida kidogo kuliko kutaka kupata sana, bei niliyopunguza tangu asubuhi mpaka sasa nimeshauza zaidi ya kilo 300 na nimezingatia huu ni mwezi wa Ramadhani sukari inatumika sana katika kuandaa vyakula mbalimbali.

“Wafanyabiashara msitumie ujanja kuonyesha kwamba sukari hakuna kwa sababu mnaharibu mipango ya Serikali ambayo inajitahidi kusikiliza kwa makini kero za wananchi,” amesema Ridhiwan.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mtendeni, Mustaquim Daruga, amesema wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam wamekuwa wakifika katika maduka yaliyopo kwenye mtaa huo likiwemo la mfanyabiashara huyo kununua sukari kutokana na kuuzwa kwa bei elekezi ya Serikali.

“Huyu bwana (Komail Ridhiwan) ametuletea sukari kwa shilingi 2,600 kwa kilo, watu walikuwa wananunua kilo kwa Sh 3,200, 3,500 na kuendelea lakini hapa tunaletewa kwa bei elekezi. Hizi zote ni jitihada za Rais Samia ameondoa ushuru na VAT, tunaomba wengine waige mfano huu.

“Tunaendelea kumshukuru Rais Samia kwa jitihada anazozifanya za kuhakikisha bei za bidhaa zinakuwa rafiki kumwezesha kila mwananchi kumudu kupata mahitaji muhimu,” amesema Daruga.

Serikali ilitangaza bei elekezi ya uuzaji wa sukari kwa rejareja na jumla nchini isiyozidi Sh 3,200 kwa kilo na kusisitiza mikoa kufuata bei hizo.

Kulingana na bei hizo Kanda ya Mashariki inayounganisha Mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani kilo moja ya sukari inapaswa kuuzwa kati ya Sh 2,700 hadi Sh 3,000 huku bei ya jumla ikiwa ni kati ya Sh 2,600 na 2,800.

Takwimu zinaonyesha mahitaji ya sukari nchini ni tani 520,000 lakini mvua kubwa zilizonyesha zilisababisha uzalishaji kushuka hadi kufikia tani 355,000 licha ya malengo yaliyokuwa yamewekwa ya kuzalisha tani 550,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles