NAIBU Rais wa Kenya, William Ruto na mtangazaji wa zamani wa redio, Joshua arap Sang, wamefutiwa mashtaka na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) baada ya kuonekana hawana kesi ya kujibu.
Majaji waliamua kwa wingi wa kura kuwa kesi ya Ruto na Sang ifutwe, wakiongeza kuwa uamuzi wao huo hauzuii kufunguliwa upya kwa kesi dhidi yao ICC au mahakama za kitaifa.
“Mashtaka yanafutwa na watuhumiwa wanakuwa huru bila kujali imani yao kwamba hawana kesi ya kujibu au haki ya upande wa mashtaka kuamua kuwafungulia upya kesi,” Jaji Kiongozi Eboe-Osuji alisema na kuongeza kwamba kulikuwa na uingiliaji wa mashahidi na kisiasa.
Majajui Eboe-Osuji na Robert Fremr, kwa pamoja walikubaliana kufutwa kwa kesi na watuhumiwa kuachiwa huru. Walitoa sababu tofauti za uamuzi wao.
Jaji Fremr alibaini kuwa hakuna kesi ya kujibu kwa watuhumiwa hao kutokana na tathmini yake katika ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka kwa mujibu wa mwongozo wa mahakama hiyo.
Aliamua kuwa upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi wa kutosha, ambao ungekiaminisha pasipo shaka chombo hicho kuwa kinaweza kuwatia watuhumiwa hatiani.
Hali kadhalika, aliona kwamba hakuna sababu ya kuita upande wa utetezi kuileta au kuiendeleza kesi hiyo.
Jaji Eboe-Osuji alikubaliana na tathmini ya Jaji Fremr, lakini alieleza kuwapo kasoro katika kesi, kwa sababu kwa mtazamo wake kuna uingiliaji wa mashahidi na siasa, ambao huenda umeathiri ushahidi wa upande wa mashtaka.
Jaji Hererra Carbuccia kwa upande wake alipingana na wenzake, ambapo kwa mtazamo wake alisema mashitaka ya watuhumiwa wote wawili hayapaswi kufutwa kwa sasa.
Kwa mujibu wa jaji huyo, kesi hiyo haijavunjika na kwamba kuna ushahidi wa kutosha, ambao iwapo utakubaliwa kutumika, mahakama inaweza kuwatia hatiani watuhumiwa hao.
Wawili hao wamefutiwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu yanayotokana na machafuko ya baada ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya 2007/2008, ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,113 na wengine zaidi ya 500,000 kugeuka wakimbizi wa ndani.
Timu za kisheria za Ruto na Sang ziliwasilisha ombi kwa majaji Septemba mwaka jana, zikisema Mwendesha Mashitaka wa ICC, Fatou Bensouda hajajenga kesi, ambayo ingewafanya waandae utetezi na hivyo kuwataka waitupilie mbali kwa vile hawana kesi ya kujibu.
Ombi hilo lilisikilizwa Januari mwaka huu, lakini majaji waliuzuia upande huo wa utetezi kuwasilisha mashahidi kuunga mkono hoja zao za kisheria.
Hata hivyo, mwezi mmoja baadaye, majaji wa rufaa walikubali rufaa yake ya kupinga kutumiwa kwa ushahidi wa mashahidi waliojiondoa, ikimaanisha ushahidi ulioandikishwa awali na upande wa mashtaka hauwezi kutumiwa dhidi ya Ruto na Joshua Sang.
Uamuzi huo ulikuwa pigo kubwa kwa upande wa mashtaka unaoongozwa na Fatou Bensouda.
Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi sita waliokuwa wanahusisha Ruto na ghasia za baada ya uchaguzi za mwaka 2007-08, walioondoa ushahidi wao.
Upande wa mashtaka umekuwa ukisema mashahidi hao walitishiwa au kuhongwa.