24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Magufuli ziarani Rwanda leo

maguuliNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Rais Dk. John Magufuli leo anatarajia kuondoka nchini kuelekea Rwanda, ikiwa ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu aapishwe kuingia madarakani Novemba 5, mwaka jana.

Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, ilieleza kuwa katika ziara hiyo Rais Magufuli na mwenyeji wake Rais Paul Kagame wanatarajia kufungua daraja la kimataifa la Rusumo na kituo cha pamoja cha ukusanyaji ushuru mpakani, ambacho ni moja ya miradi muhimu iliyoanzishwa kwa hisani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Miundombinu hiyo ambayo ipo katika mpaka wa Tanzania-Rwanda, ni muhimu si tu katika kurahisisha mchangamano baina ya nchi hizi mbili, bali pia kuunganisha zaidi ardhi zisizo na bahari katika mataifa ya Afrika Mashariki na Kati na Bahari ya Hindi.

Baada ya sherehe ya ufunguzi, viongozi hao wawili wataelekea mjini Kigali, ambako watafanya mazungumzo pamoja na kuweka shada la maua kuadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Kama mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ziara ya kwanza ya kigeni ya Rais Magufuli katika eneo hilo pia inaashiria dhamira yake ya kupanua mchakato wa uchangamano na kuimarisha uhusiano baina ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Rais Magufuli ambaye staili yake ya kubana matumizi na vita dhidi ya ufisadi, maarufu kama ‘utumbuaji majipu’ imeteka vyombo vya habari duniani, ataanza ziara hiyo ya siku mbili kwa kufungua kituo cha mpakani cha Rusumo.

Baada ya ufunguzi wa kituo hicho cha pamoja cha ukusanyaji ushuru, ambacho kinaunganisha mataifa haya mawili jirani, atafanya mkutano na waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake Rais Kagame.

Katika siku yake ya pili ya ziara hiyo ya kikazi kesho, Rais Magufuli ataungana na Wanyarwanda kote duniani kuadhimisha miaka 22 ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani.

Siku hiyo ambayo Wanyarandwa huomboleza vifo vya watu zaidi ya milioni moja vilivyotokea mwaka 1994, wengi wao wakiwa Watutsi, Rais Magufuli na mwenyeji wake Kagame pamoja na wake zao wataweka mashada ya maua na kuwasha mishumaa ya kumbukumbu.

Baada ya tukio hilo, Dk. Magufuli ataungana na Wanyarwanda katika matembezi yajulikanayo kama ‘Walk to Remember’ maalumu kwa kumbukumbu ya mauaji hayo na kuwasaidia walionusurika kabla ya kuhudhuria mkesha kwenye Uwanja wa Taifa wa Amahoro mjini Kigali.

Rais Magufuli amekuwa akitumia muda mwingi akiwa Ikulu Dar es Salaam kwa shughuli za utendaji kazi kwa Serikali yake na alisafiri mara chache nje ya jiji hilo kwenda mikoa ya Dodoma, Arusha, Mwanza, Morogoro, Singida na Geita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles