* Hamad Rashid, Amina Salum, Balozi Karume wateuliwa uwakilishi
NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, amevunja ukimya juu ya kuendelea kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pia amezungumzia ugumu wa kupatikana kwa Makamu wa Kwanza wa Rais, kwa kusema kuwa hakuna chama cha siasa kinachokidhi masharti ya kikatiba, ili kuunda Serikali hiyo.
Kutokana na kauli hiyo ya Dk. Shein ni wazi kuwa Serikali yake anayotarajia kuiunda haitokuwa na Makamu wa Kwanza wa Rais kama Katiba ya Zanzibar inavyoelekeza.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini Unguja, katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la tisa la Wawakilishi (BLW), ambapo alisema amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya baadhi ya watu kuhisi kuna mgombea wa urais anayestahili kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, baada ya uchaguzi wa marudio wa Machi 20, mwaka huu.
Alisema watu hao wamekuwa wakiibua hoja na kudai kuwa kuna mgombea anayestahili kuwa katika nafasi hiyo, lakini hataki kumteua na kudai anakiuka Katiba jambo ambalo si sahihi.
“Katika uchaguzi wa Machi 20 hakukuwa na chama chochote zaidi ya Chama Cha Mapinduzi, kilichopata matokeo ya kura za uchaguzi wa Rais kwa zaidi ya asilimia 10, mimi nilipata asilimia 91.4, hakuna chama cha siasa zaidi ya CCM chenye wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi.
“Kwa kuzingatia msingi huo na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 39 (3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, hakuna chama cha siasa kinachokidhi masharti ya kustahiki kutoa Makamu wa Kwanza wa Rais ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema Dk. Shein.
Rais huyo wa Zanzibar, alisema hatua ya kutoundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), unatokana na uamuzi uliofanywa na wananchi baada ya kuipa ushindi mkubwa CCM katika uchaguzi wa marudio.
Kutokana na hali hiyo alisema ni wananchi ndiyo wameshindwa kutoa nafasi ya kuteuliwa kwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
“Huo ni uamuzi wao wa kidemokrasia, uteuzi nilioufanya wa kumteua Makamu wa Pili wa Rais umekidhi matakwa ya kifungu cha 39(6) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
“…nililolifanya la kumteua Balozi Seif Ali Iddi kuwa Makamu wa Pili wa Rais ni sahihi na ni kwa mujibu wa Katiba na nimechukua hatua ya kuunda Serikali kwa kuzingatia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Arusha vijembe
Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein aliwapiga vijembe mahasimu wake katika siasa na kusema kwamba maneno yanayosemwa dhidi yake hayamkoseshi usingizi kwani uchaguzi umekwisha na mshindi amepatikana.
“Uchaguzi umekwisha na washindi wamepatikana ndio sisi tuliomo humu ndani na wengine nitawateua ili tuiongoze nchi kwa kipindi cha miaka mitano, hakuna tena uchaguzi mkuu mwingine, uchaguzi ushafanyika na mwingine utafanyika 2020,” alisema Dk. Shein.
Pamoja na hali hiyo aliwahakikishia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba Serikali atakayoiunda itasimamia misingi ya haki, uwajibikaji, uwazi na usawa kwa wananchi wote bila kumbagua mtu yeyote kutokana na eneo analotoka.
“Mimi ni Rais wa wananchi wote wa Zanzibar, nitashirikiana na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na viongozi wa dini, Zanzibar ni yetu sote, viongozi wa vyama vya siasa tuna jukumu la kushikamana na kuwatumikia wananchi kwa ajili ya maendeleo yao,” alisisitiza.
Vurugu
Katika hotuba yake, Dk. Shein aligusia suala la amani na kuonya hatokuwa na muhali na watu watakaojaribu kuibeza Katiba ya Zanzibar aliyoapa kuilinda ikiwa ni pamoja na kuchezea amani ya watu wa Zanzibar.
Kutumbua majipu
Dk. Shein alisema Serikali itachunguza baadhi ya viongozi na watumishi wanaotajwa na wananchi wakijihusisha na vitendo vya rushwa na kusisitiza majipu hayo atayatumbua na kuutoa kiini chake.
“Inasemekana baadhi yao wananchi wanadiriki kuvisema vitendo vya rushwa, tutawachunguza viongozi na watumishi wanaofanya vitendo hivyo, kwa kuzingatia sheria na taasisi zake ili tuujue ukweli na tuchukue hatua yapo mambo hayo yanayofanyika, ndio hayo yanayoitwa majipu nitayatumbua na moyo wake nitautoa,” alisema.
Baraza la Wawakilishi lina wajumbe 78 wote kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo 54 ni wa majimbo ya uchaguzi na 22 ni wa Viti Maalumu pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na Spika wa Baraza la Wawakilishi.
Baraza la Mawaziri
Dk. Shein aliwataka mawaziri atakaowateua kuwa wabunifu na kutosubiri kupata maelekezo kutoka kwake au kwa Makamu wa Pili wa Rais ili kwenda na kasi inayotakiwa.
“Lazima waifanye kazi ya kuwasimamia watumishi walio chini yao na wale watakaozikiuka sheria na taratibu watapaswa wawachukulie hatua na kuwawajibisha, kama hawatafanya hivyo, basi na wao watawajibishwa,” alisema.
Hamad Rashid, Balozi Karume wateuliwa
Saa chache baada ya kuzindua Baraza la Wawakilishi, Dk. Shein, alitangaza uteuzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Uteuzi huo ameufanya kwa mujibu Katiba kifungu cha 66 cha Katiba ya mwaka 1984.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Zanzibar, ilieleza kuwa Dk. Shein amemteua Mohamed Aboud Mohamed, Amina Salum Ali, Moudline Castico na Balozi Ali Karume.
Wengine ni waliokuwa wagombea urais wa vyama vya upinzani ambao ni Hamad Rashid Mohamed (ADC), Said Soud Said (AFP) na Juma Ali Khatib (Ada-Tadea).