MOFISA watendaji wa kata na vijiji wilayani Hai wameagizwa kuhakikisha tatizo la upungufu wa madawati katika shule za msingi na sekondari liwe limekwisha ifikapo Aprili 30 mwaka huu.
Agizo hilo lilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Said Mderu, alipozungumza na maofisa hao na wakuu wa shule za msingi, sekondari, waratibu elimu kata na wakuu wa idara wilayani humo kuwahimizi juu ya uwajibikaji kazini.
Alisema kutokana upungufu mkubwa wa madawati wilayani humo, watendaji hao wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanalidhbiti tatizo hilo haraka iwezekanavyo.
“Katika shule za sekondari na msingi katika halmashauri yetu tunakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati kutokana na ongezeko la wanafunzi, hivyo nawaagiza mhakikishe ifikapo Aprili 30 mwaka huu tatizo hilo liwe limekwisha,”alisema Mderu.
Alisema katika utekelezaji wa agizo hilo ofisi yake imenunua mbao zaidi ya 1,000 za awamu ya kwanza za kutengeneza madawati 2,000 na kila ofisa mtendaji hana budi kutumia njia mbalimbali kufanikisha azma hiyo.
“Ni vema mkatumia njia mbalimbali ikiwamo kuwaomba wahisani wa ndani na nje ya wilaya kusaidia kuondoa tatizo la madawati kwa vile kwa sasa hii ndiyo changamoto kubwa,” alisema.