27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Uhuru Kenyatta ahaha bomba la mafuta

keneyttra

*Ni lile litakalojengwa Tanga kwenda Uganda

*Aenda Ufaransa kukutana na viongozi wa Total

Mwandishi Wetu na mashirika ya habari

RAIS Uhuru Kenyatta wa Kenya  aliondoka  nchini mwake jana asubuhi kwenda Ufaransa na Ujerumani kwa ziara ya  kazi ambayo pamoja na mambo mengine itahusisha suala la ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda.

Kenya hivi karibuni  imeingia katika mvutano na Uganda,  ikiitaka jirani yake huyo kurudisha mpango wa kulipitisha bomba hilo la mafuta nchini humo (Kenya) badala ya Tanzania.

Suala hilo ni sehemu ya ajenda ya  biashara, ushirikiano na maendeleo ambayo ni moja ya malengo ya ziara ya Rais Kenyatta.

Kituo cha kwanza cha ziara ya Rais Kenyatta kitakuwa Paris,   Ufaransa, kuanzia leo Aprili 4 hadi 6 kabla ya kuelekea Berlin, Ujerumani atakakokaa hadi Aprili 8, mwaka huu.

Itakuwa ni mara ya kwanza katika  miaka 17 kwa Rais wa Kenya kuitembelea Ujerumani.

Mara ya mwisho, ziara ya aina hiyo ilifanywa na Rais Daniel arap Moi mwaka 1999 huku Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, akiitembelea Kenya mwaka 2011.

Ziara nchini Ufaransa kwa mujibu wa Ikulu ya Kenya, imeandaliwa na wizara ya mambo ya nje kwa mwaliko wa Rais François Hollande.

BOMBA LA MAFUTA

Ziara ya Ufaransa inatarajia kuipa Kenya fursa ya kuzungumzia suala la ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda, ikilenga kuiomba serikali ya nchi hiyo kutia mkono wake  kufanikisha azma yake ya ujenzi wa bomba hilo. Kenye inahesabu imeporwa na Tanzania mradi huo.

Kampuni ya Total ya Ufaransa ni mwanahisa mkubwa wa uwekezaji wa mafuta  Uganda na inaaminika ndiyo iko nyuma ya uamuzi wa hivi karibuni wa Uganda kuachana na mpango wa ujenzi wa bomba hilo kutoka njia ya Hoima- Lokichar- Lamu  ya  Kenya na badala yake kulijenga hadi katika bandari ya Tanga,   Tanzania.

Tofauti na washirika wengine wa uwekezaji huo kutoka Uingereza na China, Total mara kwa mara imekuwa ikisisitiza ujenzi wa bomba hilo kupitia njia ya Kusini nchini Tanzania kwa kile inachosema unafuu na usalama kulinganisha na Kenya.

Tayari mmoja wa viongozi wake waandamizi amemtembelea Rais John Magufuli Ikulu,  Dar es Salaam na kumhakikishia dhamira ya kampuni hiyo pamoja na kupatikana  kwa fedha za ujenzi huo.

Kampuni hiyo pia imetoa tamko jingine hivi karibuni wakati wa mkutano wa wadau wa nishati Afrika Mashariki uliofanyika Dar es Salaam, ikisema inajua jitihada zinazofanywa na Kenya kutaka bomba hilo lijengwe nchini humo, lakini msimamo wake wa kujengwa Tanzania uko pale pale.

Kwa mujibu wa taarifa za Ikulu, Ufaransa iko katika nafasi ya sita kama mmoja wa wawekezaji wakubwa   Kenya.

Uwekezaji huo unaanzia sekta ya uchukuzi, ufamasia, magari na sekta ya huduma zikiwamo SDV-Transami, AGS, Frasers Schneider, Peugeot, Renault, Michelin na Proparco.

Wawekezaji wengine ni   Total Kenya, Bamburi Cement, Alcatel, na kampuni ya mawasiliano ya Ufaransa Telecom yenye ubia na Telkom Kenya na Orange Mobile.

Kwa mujibu wa mpango wa ziara nzima, Rais Kenyatta akiwa Ujerumani atakuwa na  mkutano na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.

Miongoni mwa masuala ya kujadiliwa nchini humo ni pamoja na biashara, uwekezaji na ushirikiano katika usalama, utamaduni na elimu, utalii, amani katika kanda na migogoro ya Sudan Kusini na Burundi.

MASLAHI YA UFARANSA

“Ufaransa imeeleza kutaka kukuza ushirikiano na Kenya katika masuala ya kupambana na ugaidi na masuala ya itikadi kali,” taarifa hiyo fupi ilisema na kuongeza:

“Inatarajiwa kuwa wakati wa ziara Rais Kenyatta si tu atajadili masuala hayo na Rais Hollande bali pia atatembelea Kituo cha Udhibiti wa Migogoro Ufaransa na makao makuu ya taasisi za usalama za Ufaransa   kujifunza namna Ufaransa inavyokabiliana na masuala ya usalama”.

Rais Kenyatta na Rais Hollande watazungumzia pia masuala ya amani na usalama katika Pembe ya Afrika hasa Somalia, kupambana na ugaidi na itikadi kali na uwekezaji baina ya mataifa hayo, utalii na ushirikiano katika sekta mbalimbali kama vile nishati, afya, elimu, kilimo, maji, michezo na utamaduni.

Hivi karibuni Ufaransa ilikumbwa na matukio ya ugaidi kama ilivyotokea   Kenya mwaka uliopita, ingawa hadi sasa vimekuwapo  vitisho  kadhaa vya ugaidi.

Kwa Kenya, shambulio la karibuni liliikumba kambi ya Jeshi la Ulinzi la Kenya huko El Adde, Somalia, Januari mwaka huu, ambako askari wengi waliuawa.

Kwa upande mwingine, shambulio baya zaidi kuikumba Ufaransa katika historia lilitokea  Paris Novemba mwaka jana ambako watu 130 waliuawa.

Ufaransa pia iliahidi kutoa Sh milioni 11.5 za Kenya kusaidia elimu na waathirika wa shambulio la ugaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa mwaka jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles