25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 9, 2024

Contact us: [email protected]

Bandari yasaka meli 65 zilizotoweka

DARPORTNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA) imesema   inatafuta taarifa   kuweza kubaini meli zaidi ya 65 zilizoingia  na kushusha mizigo nchini bila kulipa kodi.

Hiyo ni baada ya Rais Dk. John Magufuli, kueleza madudu aliyoyakuta ndani ya Bandari ikiwamo jinsi meli 65 zilivyoingia na kushusha mizigo bila kulipa ushuru wa Serikali.

Akizungumza na MTANZANIA mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Gladson Urioh,   alisema  tangu   Rais Magufuli alipotoa kauli hiyo hivi karibuni akiwa wilayani Chato, Mamlaka imekuwa ikifuatilia taarifa hizo.

“Hili suala la meli zaidi ya 65 kuingia na kutolipa kodi tunalifuatilia kwa undani sisi TPA pamoja na wadau wote vikiwamo vyombo vya ulinzi.

“Bandari ina wadau wake ambao ni pamoja na vyombo vya ulinzi, Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na Nchi kavu (Sumatra), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Chakula (TFDA), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Idara ya Uhamiaji, Idara ya Afya na Mkemia Mkuu wa Serikali na wengine.

“Tunaamini kwa umoja wetu huu tutapata taarifa kwa undani  kuhusu  suala hili la meli,” alisema Urioh.

Akizungumzia   uwekezaji wa bandari nchini, alisema kwa sasa TPA ipo katika mkakati wa ujenzi wa gati kubwa la kisasa katika Bandari ya Mtwara ambalo litakuwa na uwezo mkubwa.

Alisema ujenzi wa gati hilo utagharimu Sh bilioni 200 na fedha za ujenzi zitatolewa na TPA kwa asilimia 100 na si za mkopo wala wahisani.

“Tumekuwa tukifanya juhudi mbalimbali ikiwamo kuhakikisha bandari zetu zinakuwa za kisasa, ingawa tuna jukumu la kusimamia bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara… bandari inayojiendesha kwa faida kidogo ni ya hapa Dar es Salaam pekee,” alisema Urioh.

Mkurugenzi huyo   alisema Mamlaka ina jukumu la kuhakikisha inasimamia kwa ufanisi bandari kubwa pamoja na zile zilizopo kwenye maziwa makubwa nchini na imekuwa ikijitahidi kuziendesha kwa ufanisi.

Kauli ya Magufuli

Wiki iliyopita akiwa wilayani Chato, Rais Dk. John Magufuli, alifichua zaidi madudu ndani ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) akieleza jinsi meli 65 zilivyoingia na kushusha mizigo nchini bila kulipa ushuru wa Serikali.

Alisema meli hizo zilishusha mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na baada ya kupakua mizigo hiyo ziliondoka  bila kujulikana zimekwenda wapi.

Kutokana na hali hiyo alisema sasa atalazimika kuchukua hatua za kurejesha nidhamu kwa watumishi wa Serikali.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara wilayani Chato, Rais Magufuli alisema ni jambo la aibu kwa nchi kuendelea kukosa mapato kwa uzembe wa watu wachache.

“Ndugu zangu tusipochukua hatua nchi itatushinda leo (juzi) pale bandari zimeingia zaidi ya meli 65 zimeshusha mizigo na hazikuonekana, hivi inawezekana vipi meli ishushe mizigo na kutokomea bila kulipa mapato ya Serikali?

“Meli zilileta mizigo zikashusha na zikapotea hivyo hivyo na Serikali ikakosa hela. Jamani ndani ya Serikali kuna madudu ya kila aina hivyo ninawaomba mniombee, nimejitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa.

 

Bandari ya Mwambani

Akizungumzia   ujenzi wa Bandari ya Mwambani mkoani Tanga, Urioh, alisema  awamu ya kwanza   imekamilika na kinachofuata   ni kutangaza tenda ya ujenzi wa bandari kwa mujibu wa sheria.

“Awamu ya kwanza ilikuwa ni kufanya maandalizi  na michoro kwa ajili ya bandari ya Mwambani. Na hili ni pamoja na kulipa fidia kwa wananchi.

“… baada ya kukamilika   michoro hiyo pamoja na taratibu zake tunajiandaa kutangaza tenda ya ujenzi wa bandari hii na hili litakaribisha kufungua milango kwa wabia ambao kama watakuwa wako tayari tunawakaribisha pia,” alisema Urioh.

Majipu bandarini

Waziri Mkuu, Khassim Majaliwa naye amekwisha kufanya ziara kwenye Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ambako alibaini mambo mengi hayaendi vizuri na kulazimika kuchukua hatua mbalimbali zikiwamo kuwajibisha watendaji.

Majaliwa alipofanya ziara ya kushitukiza katika bandari ya Dar es Salaam, aligundua kontena 329 zilipitishwa bila kulipiwa kodi kinyume na utaratibu wa bandarini.

Katika  mkakati wa Serikali ya awamu ya tano ya kutumbua majipu, Rais Magufuli alivunja bodi   ya bandari siku chache baada ya kupatikana   kontena ambazo hazikuwa zimelipiwa ushuru katika bandari ya Dar es Salaam huku kampuni 43 zikigunduliwa kuhusika katika makontena hayo.

Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Joseph Msambichaka  na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Awadhi Massawe walivuliwa nyadhifa zao.

Pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka aliondolewa kwenye wadhifa huo.

Waziri Mkuu, hivi karibuni alifanya ziara ya kushitukiza katika Bandari ya Tanga ambako pamoja na masuala mengine, alikuta tishali tatu zikiwa chakavu bila ya injini wakati serikali ilitoa fedha za ununuzi wa matishali ya kisasa.

Baada ya kubaini jipu hilo, alimwagiza Meneja wa Bandari ya Tanga, Henry Arika, kutoa maelezo kwa maandishi ya nani alihusika na ununuzi wa matishali hayo badala ya zile mbili zilizopaswa kuwapo ambazo Serikali ilitoa dola za Marekani milioni 10.

Arika alijitetea akisema kwamba tishari hizo ziliwasili nchini miaka minne iliyopita iliyopita lakini zilianza kufanya kazi rasmi mwaka jana na kwamba yeye hana muda mrefu katika bandari hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles