Na Mwandishi wetu
Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Uchukuzi na Utalii wa Japan, Konosuke Kokuba anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini mnamo Januari mwaka 2024 akiwa na ujumbe wa watu 40.
Watu atakaongozana nao Kokuba ni kutoka kampuni binafsi zinazojihusisha na masuala ya miundombinu na baadhi ya watumishi wa wizara yake.
Ziara hiyo imelenga kujadili fursa mbalimbali zinazotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika maendeleo ya miundombinu.
Kikao cha pamoja cha maandalizi ya ziara hiyo kimefanyika Desemba 7, 2023, jijini Dar es Salaam kilichoshirikisha viongozi wa Wizara ya Uchukuzi akiwamo Katibu Mkuu Profesa Godius Kahyarara na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa pamoja na menejimenti yake.
Kwa upande wa Japan, ujumbe wake uliongozwa na Yoshihiro Kakishita kutoka Sekretarieti ya Wizara ya Ardhi, Miundombinu, Uchukuzi na Utalii ya Japan.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mbossa ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Japan kuja kuwekeza kwa upande wa miundombinu ya Bandari nchini.