Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Baada ya Serikali kuruhusu jengo la Kanisa la Spirit Word Ministry lililopo Stakishari Ukonga jijini Dar es Salaam kutumika kwa shughuli nyingine za kijamii, viongozi wake wameiangukia Serikali wakiomba waruhusiwe kutoa huduma za kiroho.
Mei 2023 Serikali ilitangaza kusitisha huduma za kanisa hilo lililo chini ya Askofu Dk. Ceasar Masisi na mkewe, Dk. Elizabeth Kilili, kwa kile kilichoelezwa kuwa linachochea mapenzi ya jinsia moja.
Akizungumza Novemba 29,2023 na waandishi wa habari, Dk. Kilili amesema Serikali imewaruhusu kutumia jengo kwa shughuli nyingine za kijamii.
“Tunaishukuru Serikali yetu sikivu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia haki, tunatoa tamko kuwa hatuna uhusiano wowote na wanaotetea mapenzi ya jinsia moja.
“Baada ya uchunguzi Serikali imeruhusu jengo la kanisa liweze kufunguliwa na kutumika kwa shughuli nyingine za kijamii, hii ni changamoto kubwa kwetu pamoja na waumini wote wa SWM…tunaiomba Serikali ituruhusu tuendelee kutoa huduma za kiroho,” amesema Dk. Kilili.
Amesema wamekuwa wakihubiri neno la Mungu na kutoa mafundisho yanayolenga kujenga maadili ya Watanzania na kwamba hawajawahi kuhamasisha mapenzi ya jinsia moja kama inavyodaiwa.