Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ameitaka
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (TCAA), kuhakikisha wanasimamia ubora wa miradi ili imalizike kwa wakati.
Kauli hiyo ameitoa leo Novemba 22, 2023 jijini Dar es Salaam, alipotembelea Ofisi za mamlaka hiyo kwa lengo la kufahamiana na kupata fursa ya kuonana na Menejimenti na kujua mpango wa wafanyakazi wake.
Kihenzile amesema haikubaliki mradi wa mwaka mmoja unashindwa kumalizika kwa wakati uliopangwa.
“Muendelee kusimamia ubora wa miradi hii iweze kukamilika kwa wakati na thamani ya fedha zilizotolewa, muweke utaratibu mzuri wa kusimamia maelekezo yaliyotolewa na viongozi yawe na mfumo wa utekelezaji,” amesema Kihenzile.
Ameagiza pia TCAA kusimamia mashirika yao ya ndege ya ndani na nje ili kudhibiti ajali na kutafuta ufumbuzi wa malalamiko ya wananchi ikiwamo kuahirisha safari.
“Zaidi ya mabilioni yameelekezwa katika miradi na bado Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatenga fedha ili kuhakikisha usalama wa vifaa vya mbalimbali vya angani ambavyo kimsingi vina dhibitiwa na vina simamiwa na TCAA,”amesema.
Aidha amesema ipo miradi kadhaa mikubwa ambayo inafanyika kati yake ni ujenzi wa chuo cha usafiri wa anga ambacho kinafundisha watu mbalimbali.
“Tumeelezwa katika vyuo tisa bora barani Afrika cha TCAA ni mojawapo na duniani vipo 35 tu. Rais Dk .Samia anapanga utaratibu wa kutenga fedha ili kuendelea kuwekeza zaidi kujenga chuo cha kisasa kama anavyofanya kwenye sekta nyingine,” ameeleza.
Kihenzile ametoa wito kwa mashirika, wawekezaji, wafanyabiashara waingie kwenye usafiri huo, kwa kuwa ndani nan je ya nchi usafiri wa anga ni salama.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (TCAA),Hamza Johari, amesema naibu waziri huyo ameridhishwa na kazi ambazo wanafanya.
“Naibu Waziri ametoa maelekezo ikiwemo katika suala zima la miradi kuhakikisha kwamba wanafanya miradi hiyo kwa viwango na ubora unatakiwa na inamalizika kwa wakati,” amesema Johari.
Amesema miradi wanayoendelea nayo kwa sasa ni wa kubadilisha mifumo ya sauti, kuboresha mawasiliano na mradi wa ujenzi wa chuo cha usafiri wa anga.
Amesema katika miradi hiyo yote mitatu watahakikisha maelekezo waliyopewa yatayafanyia ili kufikia viwango vya kimataifa.
Aidha amesema katika kuongeza mashirika ya ndege, wanaamini itasaidia na gharama za nauli zinapungua.