Na Safina Sarwatt, Kilimanjaro
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kaskazini imevitaka vyombo vya habari kuongeza weledi na ufanisi katika uzingatiaji wa sheria na taratibu zilizopo ikiwemo leseni na maudhui ili kuweza kufikia malengo ya kuhabarisha umma.
Hayo yamebainishwa mapema leo Novemba 20, na Mkuu wa TCRA Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Imelda Salum, katika kikao na wamiliki, wasimamizi wa vyombo vya habari na waandishi wa habari mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kikao hicho kilichokuwa na lengo la kukumbusha na kujadili namna bora ya utoaji wa taarifa mbalimbali kati ya mamlaka na watumiaji huduma.
Mhandisi Imelda amesema kutokana na mabadiliko ya kidigitali TCRA imeendelea kutumia mifumo ambayo inarahisisha mteja kupata taarifa kwa haraka zaidi pamoja na kuwasilisha malalamiko ambao ni (Tanzanite Portal) na dawatilahuduma.tera.go.tz
Amesema dhumuni la TCRA ni kuhakikisha inakua kiungo muhimu kati yake na watumiaji wa huduma ili kutoa huduma bora na iliyokusudiwa ikiwemo kufika ofisi za TCRA ama kupiga simu bure 0800008272 pamoja na kuandika barua.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari wameshukuru elimu iliyotolewa na TCRA huku wakihimiza wenzao kujiunga katika umoja wa wamiliki wa radio NIBA ili kujadili changamoto za pamoja na kuziwasilisha mamlaka husika.