TIMU ya Yanga leo itakuwa na kibarua kizito cha kuendeleza makali yake wakati itakapopambana na Ndanda FC katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo unafanyika baada ya timu hiyo kufanya vizuri kwenye michezo yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuziondosha timu za Cercle de Joachim ya Mauritius na APR ya Rwanda.
Yanga itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu hiyo, walioupata katika mchezo wa 14 wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hata hivyo, timu hiyo inayosubiri kucheza dhidi ya Al Ahly wiki ijayo katika hatua ya 16 bora, itakuwa na kibarua kigumu kupata ushindi katika mchezo huo kwa kuzingatia kiwango kilichooneshwa na Ndanda katika mchezo wao dhidi ya Geita Gold Sport, wakati wa mchezo wa kufuzu hatua ya robo fainali.
Kuelekea katika mchezo huo kesho, Yanga ina wachezaji watano majeruhi ambao ni akiwamo Said Makapu, Malimi Busungu, Geofrey Mwashiuya, Deus Kaseke na Kelvin Yondani. Tofauti na Ndanda ambayo inaonekana kuwa imara kwa wachezaji wake kutosumbuliwa na majeruhi yeyote hadi sasa.
Faraja pekee kwa Yanga ni kurejea kwa washambuliaji wake mahiri ambao wanatarajiwa kuwapo kwenye mchezo huo, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na beki nguli wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Kocha msaidizi wa timu ya Yanga, Juma Mwambusi, alisema licha ya kikosi cha timu yake kuwa majeruhi watajitahidi kuwatumia wachezaji walio wazima ili kupata ushindi.
Nao wawakilishi wa kimataifa wa michuano ya Shirikisho Afrika, Azam FC watakuwa uwanjani leo kuvaana na timu ya Tanzania Prisons ya Mbeya katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Akizungumzia mchezo huo, Msemaji wa klabu hiyo, Jafary Iddy, alisema watautumia kujiandaa kabla ya kucheza dhidi ya Esperance ya Tunisia.
“Licha ya kuwa na kibarua kikubwa dhidi ya Prisons, tutatumia mchezo huu kama chambo ya kukiimarisha kikosi chetu kuelekea mchezo dhidi ya Esperance,” alisema.
Hata hivyo, mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa kwenye Ligi Kuu ambapo historia iliendelea kuitafuna Azam FC kwenye Uwanja wa Sokoine baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya wenyeji wa mchezo huo Prisons ‘Wajelajela’.
Mbali na kutopata matokeo mazuri kwenye uwanja huo tangu zikutane, safari hii Azam itakuwa mwenyeji wa Prisons Uwanja wa Azam Complex. Huenda Azam ikatumia vema uwanja wake wa nyumbani ambapo katika mechi tatu za Ligi Kuu msimu huu imeshinda zote.
Prisons katika michezo mitatu dhidi ya Azam, miwili kati ya hiyo imeshinda ikiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani Sokoine na kutoa sare mmoja ikiwa ugenini.
Timu zote zimetoka sare mara tano kati ya michezo 11 ya Ligi Kuu tangu Azam ilipofanikiwa kupanda ligi kuu, michezo sita iliyobaki kila timu imeshinda mitatu.