24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wachezaji Mbeya City wagoma

Mbeya-City-KikosiNa Pendo Fundisha, Mbeya

WACHEZAJI wa klabu ya Mbeya City, wamegoma kufanya mazoezi kwa siku kadhaa na kuendelea kubaki kambini wakiushinikiza uongozi wa klabu hiyo kuwalipa mishahara yao.

Imeelezwa kwamba wachezaji hao wamekuwa wakiidai Halmashauri ya Jiji la Mbeya mishahara ya miezi mitatu jambo linalotajwa kuwa chanzo cha wachezaji kukosa morali ya kucheza vizuri uwanjani.

Wakizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa majina yao, baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo walisema kuwa klabu hiyo kwa sasa inakabiliwa na ukata wa fedha kwani mbali na mishahara yao pia upande wa chakula na malazi nako ni tatizo.

“Sio siri klabu yetu inakabiliwa na ukata, hali ni mbaya kwani licha ya kula chakula kisichokizuri pia mishahara yetu ni tatizo, hadi sasa huwezi amini uongozi haujatulipa mishahara kwa zaidi ya miezi mitatu,” kilisema chanzo cha habari hizi.

Chanzo hicho kilieleza kuwa ukosefu wa mishahara ni moja ya changamoto zinazoigharimu timu hiyo kufanya vibaya, kwani wachezaji wamekuwa wakifanya mgomo baridi kwa kutocheza vizuri uwanjani ikiwa na kugoma kwenda kufanya mazoezi kwa zaidi ya siku tano.

“Viongozi wakifika kuzungumza na wachezaji wamekuwa wakiwafariji tu kwa macho ila moyoni wachezaji wamejiwekea misimamo yao wenyewe, hivyo ni vema mwajiri wetu akalifahamu hili na kulifanyia utatuzi,” alisema.

Akizungumzia hilo, Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi, alikiri kwamba klabu hiyo inakabiliwa na ukata wa fedha na tayari wamezungumza na wachezaji ili kuona ni jinsi gani mishahara hiyo watalipwa.

“Kweli wachezaji wanadai mishahara yao lakini juzi tumezungumza nao na kuna kiasi cha fedha wameingiziwa, uongozi unaendelea na mchakato wa kutafuta fedha zitakazoweza kulimaliza tatizo hilo,” alisema.

Aidha, Meya huyo aliwaomba wachezaji hao kuendelea na mazoezi ya kujiandaa na mechi ngumu za mbeleni kwani timu hiyo kwa sasa ina wakati mgumu wa kuhakikisha inasimama katika msimamo wa ligi kuu.

“Timu kwa sasa ipo sehemu mbaya nilichowaomba wachezaji tushikamane na kufanya vizuri ili tujinasue katika kushuka daraja na uongozi ujipange kwa msimu ujao wa ligi kuu,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles