25.1 C
Dar es Salaam
Monday, October 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara mbili Bara na Zanzibar zasaini makubaliano

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

WIZARA za Nishati, Wizara ya Maji na Nishati na Madini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zimesaini hati ya makubaliano ya kuimarisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwamo uandaaji wa sera na sheria, utafiti kuhusu uendelezaji wa sekta ya nishati.

Makubaliano hayo pia yatahusisha , kubadilishana takwimu, uzoefu na utaalamu katika sekta hiyo.

Hati hiyo imetiwa saini na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dk. Doto Biteko kwa upande wa Tanzania Bara na Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar,Shaib Hassan Kaduara katika hafla iliyofanyika leo Novemba 12,2023 jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dk. Doto Biteko, amesema msisitizo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi hautaishia Tanzania Bara pekee bali hatua za uhamasishaji zitafanyika hadi Zanzibar.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Biteko amesema kutiwa saini kwa hati hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi ambao mara kadhaa wamekuwa wakitoa maelekezo kwa wizara hizo mbili kuwa na ushirikiano ili kuendeleza sekta ya nishati nchini.

“Viongozi wetu wakisema, kinachotakiwa kutokea ni matokeo ya kile kilichosemwa, vinginevyo tutakuwa hatuwasaidi kama wanasema na hakuna mabadiliko, ninataka niwahakikishie kwamba sisi tunathamini sana mashirikiano tuliyonayo na ushirikiano huu utakuwa endelevu,”amesema Dk. Biteko.

Amesema kuwa, makubaliano hayo yatahusisha taasisi zilizo chini ya wizara hizo mbili ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA).

Nyingine ni Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA) , Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).

“Tumesaini hati hizi si kwa ajili ya kupiga picha bali tunataka tuone matokeo yanatokea, hivyo tukafanye ufuatiliaji wa yale tuliyokubaliana, inabidi tuwe na timu ndogo za kufuatilia yale tuliyokubaliana ili mwisho wa mwaka tupime tumefika wapi,”amesema.

“Wakati wa makubaliano kumekuwa na maneno mazuri yanayozungumzwa lakini katika utekelezaji wa makubaliano tunayowekeana yanakuwa tofauti na mikataba tunayokubaliana,hivyo kwa upande wa Tanzania Bara tutahakikisha kila tulichokubaliana kinatekelezwa,” amesema Dk. Biteko.

Katika hatua nyingine Dk.Biteko amesema Wazanzibar watafaidika kama watanzania wengine kwa kupata mitungi ya gesi lengo likiwa ni kuwahamasisha kutumia nishati safi ya kupikia.

Amesema utoaji wa mitungi ya gesi itaendelea na utoaji wa promosheni ya nishati hiyo ili kurahisisha kila mwananchi anatumia mitungi hiyo.

Kuhusu umeme amesema kuwa, laini ya KV 132 inayotoa umeme Tanzania Bara kwenda Zanzibar imeshazidiwa kwani matumizi ya umeme yameshakuwa makubwa kutokana na shughuli za utalii, viwanda na matumizi mengine hivyo kwa sasa mpango uliopo ni kujenga laini ya KV 220 ili kupeleka umeme wa uhakika Zanzibar.

Akizungumzia makali ya umeme nchini, Dk.Biteko amesema yanaendelea kupungua kwani kulikuwa kuna upungufu wa megawati 810 lakini sasa umepungua na kufikia megawati 240 na imani iliyopo ni kuwa mwanzoni mwa mwaka 2024 makali ya umeme yatakuwa yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar,Shaib Hassan Kaduara amesema hati zilizosainiwa ni nyenzo za kuendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali kwenye sekta ya nishati.

Amesema kuwa, wanategemea wataalam wa Tanzania Bara na Zanzibar wataendelea kushirikiana kwenye masuala mbalimbali ikiwemo la kutatua changamoto ya upotevu wa umeme unaotokana na wizi au mambo mengine ya kitaalamu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles