26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Watahiniwa 572,338 kitado cha nne kufanya mtihani kesho

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

JUMLA ya watahimiwa 572,338 wanatarajiwa kuanza kufanya mtihani wa kidato cha nne utakaoanza kesho Novemba 13 -30, 2023, ambapo kati yao wa kujitegemea ni 8,952.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 12,2023 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA), Dk.Said Mohamed amesema kati ya watahimiwa wa shule 543,386 waliosajiliwa mwaka huu, wavulana ni 250,237 sawa na asilimia 46.05 na wasichana ni 293,147 sawa na asilimia 53.95.

“Jumla ya watahiniwa wa shule wenye mahitaji maalumu ni 614, ambao kati yao 283 ni wenye uoni hafifu, 24 ni wasioona, 135 wenye ulemavu wa kusikia ,11 ni wenye ulemavu wa akili na 161 wenye ulemavu wa viungo vya mwili,” amesema Dk.Mohamed.

“Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 28,952 waliosajiliwa, wavulana ni 11,867 sawa na asilimia 40.99 na wasichana ni 17,085 sawa na asilimia 59.01.Watahiniwa wa kujitegemea wenye mahitaji maalumu wako nane , wenye uoni hafifu ni wanne na wasioona ni wanne,”amesema.

Amesema mwaka jana, jumla ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa walikuwa 534,753 hivyo kuwa na ongezeko la jumla ya watahiniwa 8,633 sawa na asilimia 1.61 kwa mwaka huu ukilinganisha na mwaka jana.

Ameeleza kuwa mwaka huu jumla ya shule za sekondari 5,371 na vituo vya kujitegemea 1,798 vitatumika kufanyia mtihani huo.

Kuhusu mtihani wa QT

Akizungumzia kuhusu mtihani wa maarifa QT, Dk.Mohamed, amesema jumla ya watahiniwa 10,927 wamesajiliwa kufanya ambapo wanaume ni 4,020 sawa na asilimia 36.79 na wanawake ni 6,907 sawa na asilimia 63.21.

Amesema watahimiwa wa QT wenye mahitaji maalumu ni 38 ambao wote ni wenye uoni hafifu.

Amesema mwaka jana jumla ya watahimiwa waliosajiliwa walikuwa 12,110 hivyo kuwa na upungufu wa jumla ya watahiniwa 1,183 sawa na asilimia 9.77.

Amesema mtihani wa kidato cha nne ni muhimu kwa kuwa hupima umahiri wa wanafunzi katika yale yote waliyojifunza kwa kipindi cha miaka minne ya elimu ya sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne.

Dk.Mohamed ametoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zihakikishe kuwa usalama wa vituo vya mtihani unaimarishwa kwani vituo hivyo vinatumika kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na baraza.

Vilevile amewataka wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia upimaji kufanya kazi yao ya usimamizi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.

“Wasimamizi wanapaswa kuhakikisha kuwa, wanafanya kazi ya usimamizi kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mwanafunzi husika apate haki yake,”amesema

Amesema wasimamizi hao wanapaswa kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanafanya upimaji wao ipasavyo ili wapate haki yao msingi ambazo ni pamoja na kupata mitihani yenye maandishi ya nukta nudu kwa wanafunzi wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu.

Amesema baraza la mitihani halitarajii kuona mwanafunzi yoyote kujiusisha na vitendo vya udanganyifu na kutoa taadhari kuwa yoyote atakayebainika kufanya udanganyifu matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mitihani.

“Baraza linaamini kuwa walimu wamewaandaa vizuri katika kipindi chote cha miaka miwili ya elimu ya sekondari na miaka minne ya elimu ya msingi,”amesema.

Katibu huyo mtendaji amewataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya mtihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa upimaji huo.

“Baraza halitosita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo linajiridhisha pasipo shaka kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa upimaji wa kitaifa,”amesisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles