Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Makamu wa Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Phumzile Mlambo Ngcuka, amewaelekeza wanaharakati wa kifeminia nchini kujikita katika kuelimisha kuhusu ulinzi wa mtoto wa kiume kwa mustakabali wa haki na usawa wa jinsia.
Phumzile ameyabaisha hayo leo Novemba 7, 2023 jijini Dar es Salaam katika tamasha la jinsia la 15 pamoja na kuadhimisha miaka 30 Kifeminia la Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP).
Amesema katika harakati za kukataa ukandamizaji wa aina yoyote, pia suala la ulinzi wa mtoto wa kiume linatakiwa kuzingatiwa katika kuendeleza ajenda za kumkomboa.
Amesema ipo haja ya kuwa na majukwaa ya wanaume nchini yenye kueleza yanayowahusu, pia yatumike kuchukua hatua za kupinga ukatili wa kijinsia, ubaguzi dhidi ya wanawake na wanaokataa ndoa za utotoni
“Wanaharakati wa haki za binaadamu wasiruhusu aina yoyote ya ukatili kuanzia kuukataa mfumo dume katika ngazi ya familia na kuongeza kuwa ipo haja ya kuwepo mabadiliko ya kisera na sheria lakini pia jamii kubadilika,” amesema Phumzile.
Amesema mfumo dume sio rafiki kwa wanawake na hata wanaume na umekuwa ukiendeleza ubaguzi hivyo ni muhimu kwa wanaume na watoto wakiume miongoni mwa harakati za kupinga kwani hii ni karne ya wanaume wenye mshikamano na wenza wao.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gema Akilimali, amesema licha ya mtandao huo kuadhimisha miaka 15 ya usawa wa kijinsia lakini changamoto bado ni nyingi, kwa sasa wanahitaji zaidi ushirikiano na Serikali.
Gema amesema katika tamasha hilo la siku nne watatoka na maazimio ya jumla kwani upo mchango wa TGNP katika harakati mbalimbali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TNGP, Lilian Liundi amasema tamasha la jinsia ni jukwaa la kuleta sauti kwa pamoja lenye kujadili na kupanga mikakati.
“Tamasha hili ni la 15 tangu kuanzishwa limeweza kuwa na washiriki 2000 hadi 5000 kwa tamasha moja limewafikia watu zaidi ya 35000,”amesema Liliani.
Amesema tamasha hilo limewaleta watu wa ukanda wa Afrika kwa kwa pamoja na wameendelea kusimama kwenye misingi ya waasisi wao.
Aidha amesema TGNP imejengwa katika misingi imara ya haki na kuondoa mifumo kandamizi.