Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amewataka wadau na mashabiki wa timu hiyo kuwa wavumilivu na kusahau shida zote ili kupambana kutafuta matokeo ya kuwatoa katika nafasi za chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Timu hiyo imeanza msimu huu wa Ligi kwa kusuasua ambapo katika msimamo ipo nafasi ya mwisho na alama mbili ikicheza mechi sita bila kupata ushindi baada ya kutoka sare mbili na kupoteza nne.
Katwila amerejea Mtibwa Sugar hivi karibuni akitokea Ihefu FC na kesho atakiongoza kikosi hicho kilichoanza dhidi ya Geita Gold kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Kocha huyo ametaja kinachoisumbua timu hiyo ni kupata matokeo pekee bali wachezaji wako vizuri na kuweka wazi kuwa njia pekee ya kuwarejesha katika kasi yao ni kushirikiana kwa pamoja na jitihada za kupambana kwa kila hali.
“Tusahau shida zetu na tuwe kitu kimoja kwa maana katika hali kama hii lazima muwe kitu kimoja, tukiwa tofauti itazidi kutuletea shida. Mashabiki ni sehemu ya timu na mchezaji wa 12, wao watakapokuwa pamoja na sisi, wanaweza kutusapoti na kutupa ari katika kipindi hiki kigumu,” amesema Katwila.
Ameeleza kuwa tangu amefika katika timu hiyo kwa siku chache ameweza kuimarisha baadhi ya sehemu na anaamini mchezo wa kesho kutakuwa na mabadiliko.