Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Baada ya kufanya vizuri mwaka jana, tamasha la Imba Together linatarajia kufanyika tena Oktoba 27 na 28, 2023 katika miji ya Winston Salem, North Carolina huko Marekani.
Imba Together ni miongoni mwa matukio yanayoigusa jamii ya Kitanzania chini ya Muandaaji Anna Simtaji (AJS) tangu mwaka 2017 mpaka leo limeendelea kugusa watu wenye uhitaji.
Akizungumza na mtanzania.co.tz muandaaji wa Imba Together, Anna Simtaji, amesema mwaka 2019 hadi 2021 walisimama kufanya Gospel Concert na badala yake walielekeza nguvu zao kwenye jamii kwa kusaidia wajasiliamali wadogo.
“Msimu wa Corona tulisaidia wajasiliamali wadogo maeneo ya Karume, Mbagala, Makumbusho kwa kuwapa vitendea kazi kama vile ndoo kubwa za kunawia, Sanitizer, maski na elimu yaani kwa kifupi Imba Together tunarudisha kwa jamii,” amesema Anna.
Ameongeza kuwa kupitia Imba Together wameweza kujenga darasa pamoja na kununua mashine za kushonea (vyerehani) ili kusaidia wanafunzi wenye usonji (autism).
“Pia tumesaidia shule ya Msimbazi Autism, Uhuru Maalum kwa kuwapa madaftari, kalamu, nguo za watoto na vyakula kwa wazazi wao,” amesema Anna.
Mbali na kusaidia jamii Imba Together mwaka huu imejipanga kivingine kwaajili ya kumwongezea mwanamke uwezo kupitia semina ya ‘A Women of Dignity’ na tamasha kubwa la uimbaji kutoka kwa mastaa kibao wa muziki wa Injili.
“Imba Together 2023 itaanza Oktoba 27 siku ya Jumamosi kwa mkutano wa wanawake kuhusu, ‘A Women of Dignity’ kutakuwa na wanenaji wengi kama vile Pastor Dupe, Pastor Grace Josephat Gwajima, Bishop Nyisake Chaula na wengineo pia siku ya Jumamosi Oktoba 28, ndio itakuwa ile Live Gospel Concert kwa watu wote na waimbaji wakubwa Afrika watakuwepo kama vile Chris Shalom kutoka Nigeria, Christina Shusho kutoka Tanzania, Gloria Muliro wa Kenya huku Host nikiwa mimi mwenyewe, kwa mtu atakayeshiriki hii atachangia $25 kwa mtu mmoja (silver) na dola 80 kwa mtu mmoja (gold) mambo yote yatafanyika hapa hapa Winston Salem, North Carolina,” amesema Anna.