Na Mwandishi wetu,Dodoma
TUME ya Madini imesema mwelekeo wa sekta ya Madini kwa mwaka 2023-2024 ni kuhakikisha mchango wa Pato la Taifa unafikia asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa, Agosti 18,2023 na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Ramadhan Lwamo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo kwa kipindi cha mwaka 2023-2024 na mikakati kwa Waandishi wa Habari.
Kaimu Katibu Mtendaji huyo amesema mwelekeo wa sekta ya hiyo ni kuhakikisha mchango wa Pato la Taifa unafikia asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025.
Amesema kama iliyofafanuliwa katika dira ya Maendeleo ya Taifa na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja ya mpango mkakati wa Tume hiyo wa mwaka 2019-2020 hadi 2023-2024.
Amesema katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa tume inatarajia kuwa na mikakati kuimarisha usimamizi na udhibiti katika maeneo ya uzalishaji wa madini.
Pia, kuimarisha udhibiti wa biashara haramu ya madini kwa kuhamasisha umuhimu wa kutumia masoko na vituo vya madini nchini.
Vilevile, kuimarisha ukaguzi katika shughuli za uchimbaji katika migodi kwa lengo la kuwa na uchimbaji endelevu unaozingatia usalama, afya na mazingira.
“Kuimarisha shughuli za utafiti zinazohusiana na utambuzi wa vyanzo vipya vya mapato yatokanayo na rasilimali za Madini,”amesema Kaimu Mtendaji huyo.
Hata hivyo, amesema bado wanakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa sheria za Madini sura ya 123 na kanuni zake kwa wachimbaji na wafanyabiashara na umma hivyo kusababisha uwepo wa migogoro ya mara kwa mara.
Amesema wanaendelea kutoa elimu ili kutatua changamoto hiyo kwa kufika katika maeneo ya wachimbaji wadogo na viongozi wa Serikali za Mitaa.