26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, November 21, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani, Zanzibar wazindua kampeni ya ugawaji vyandarua vyenye dawa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani imezindua kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa yenye kaulimbiu ya: Usingizi Bul Bul (‘Usiku wa Amani’) ambayo itasambaza vyandarua vyenye dawa takriban 248,000 katika Shehia 53 za Unguja Zanziba, na kuonyesha maendeleo makubwa katika mapambano dhidi ya malaria.

Aidha, Shehia zilizosalia za Zanzibar zitapokea vyandarua mwaka 2024.

Kupitia ufadhili wa Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI), Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) kupitia mradi wake wa Breakthrough ACTION kwa kushirikiana na Programu ya kumaliza Malaria Zanzibar (ZAMEP) wamekuja na kampeni ya Usingizi Bul Bul, ambayo inazingatia hatua tatu muhimu:

Kwanza ni kuhakikisha kaya zinajiandikisha kikamilifu ili kupata vyandarua vyenye dawa; kuhakikisha kaya zinapokea vyandarua vyao; na kuhakikisha watu wanalala ndani ya vyandarua vilivyotiwa dawa kila siku.

AkizungumzaJulai 25, 2023 wakati wa hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vyandarua kwenye kaya, Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema, “Kampeni hii inaonyesha nia yetu kama Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa kushikiana na Mpango wa Rais wa Marekani wa kupambana na Malaria (PMI) katika kutumia mfumo wa kidigitali ili kuboresha huduma za usajili na ugawaji wa vyandarua vyenye dawa kwenye kaya.

“Tunatoa shukrani zetu kwa USAID/PMI na washirika wote kwa mchango wao usioweza kuelezeka. Kwa pamoja, tuna imani kuwa juhudi hizi za pamoja itatupeleka kufikia malengo ya Zanzibar isiyo na Malaria,” amesema Mazrui.

Amesema kwa mara ya kwanza hapa Zanzibar, mfumo wa kidigitali wa usajili na utoaji wa vyandarua umewasilishwa ili kusaidia watu kufanya usajili wa kaya zao na kupokea vyandarua kwa urahisi na kupunguza kadhia za kusubiri foleni ili kupata huduma.

Mradi wa Digital Square, unaofadhiliwa na USAID, kwa kushikiana na ZAMEP wametengeneza mfumo wa kidigitali unaorahisisha usajili na ugawaji wa vyandarua vyenye dawa ili kupunguza kucheleweshwa kwa usambazaji na kuhakikisha kuwa watu wengi wananufaika na vyandarua hivi vyenye dawa.

“Kupitia kampeni ya Usingizi Bul Bul inayotekelezwa wakati wa usajili na ugawaji wa vyandarua kwenye jamii inadhihirisha dhamira yetu kama nchi ya kutokomeza Malaria Zanzibar,” alisema Anna Hoffman, Kaimu Mkurugenzi wa Ofisi ya Afya ya USAID/Tanzania na kuongeza kuwa:

“Marekani itaendelea kutoa ushikiano na Serikali ya Zanzibar katika jitihada za kutekeleza hatua mbalimbali zinazolenga kutokomeza Malaria Zanzibar. Kupitia uzinduzi huu tunawahimiza Wazanzibari kuvipokea vyandarua hivi vyenye dawa na kulala ndani ya chandarua kila siku kwa ‘Usingizi Bul Bul,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles