Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Serikali imetenga Sh bilioni 41 kutatua kero ya maji katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Segerea ambayo yanakabiliwa na changamoto hiyo kwa muda mrefu.
Maeneo hayo ni Bonyokwa, Msingwa, Kisiwani, Mibega, Kifuru Majoka na Kinyerezi.
Akizungumza Julai 23,2023 na wananchi wa jimbo hilo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu, amesema mradi huo utakaohusisha ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita milioni 9 utatekelezwa kwa miezi 18.
Mtendaji huyo alikuwa akizungumza kwa simu katika mkutano wa hadhara baada ya kutakiwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abasi Mtemvu, kueleza namna walivyojipanga kutatua kero ya maji katika maeneo hayo.
“Wiki ya pili ya mwezi wa nane tutasaini mkataba na tutatafuta mkandarasi ambaye atafanya kazi kwa haraka zaidi ili mradi ukamilike kwa wakati…hizi ni fedha za Benki ya Dunia ambazo mheshimiwa Rais amesaidia kuzipata,” amesema Kingu.
Amesema kwa sasa wanaendelea kuongeza msukumo wa maji kukabili changamoto ya uhaba wa maji katika maeneo husika.
Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, aliandaa mkutano huo kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa mwaka 2020/23 na kutaja changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa maeneo hayo.
Amesema miradi yenye thamani ya Sh bilioni 28 imetekelezwa katika jimbo hilo ambayo inahusisha sekta za elimu, afya na miundombinu.
“Tunamshukuru sana mheshimiwa Rais na Serikali kwa mambo makubwa inayofanya katika jimbo letu la Segerea, tumejipanga kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 mambo ambayo tumeahidi tuwe tumetekeleza,” amesema Bonnah.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amesema wanafuatilia kwa karibu viongozi wa Serikai ili watekeleze miradi yote iliyopangwa.
“Tunaifuatilia kwa karibu Serikali ili 2024/25 tuweze kuwa na majibu sahihi kwa wananchi wetu. Tunaomba muendelee kutuamini na kutupa kura nyingi katika uchaguzi wa rais, wabunge, madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa,” amesema Sidde.