KIUNGO wa timu ya Arsenal, Mesut Ozil, amekanusha uvumi kwamba ataondoka katika kikosi hicho kama kocha Arsene Wenger ataendelea kuwepo.
Ozil amedai kwamba kwa sasa yupo katika klabu hiyo kutokana na uwepo wa kocha huyo na uhusiano wao kuwa mzuri.
Mtandao wa Don Balon wa nchini Hispania, ulitoa taarifa kwamba, mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Ujerumani amechoka kuitumikia Arsenal kutokana na kukosa mafanikio katika Ligi Kuu nchini England kwa muda mrefu na amepanga kurudi Hispania katika La Liga.
Habari hiyo imemfanya Ozil ajisikie vibaya, ila amedai kwamba hakuna ukweli wowote juu ya kauli hiyo na anamheshimu kocha wake, Wenger.
“Nashangaa kuona vyombo vya habari vikiandika mambo ambayo hayana ukweli, ninamheshimu Wenger na nipo Arsenal kwa ajili yake,” alisema Ozil.
Mchezaji huyo alijiunga na klabu hiyo 2013, akitokea Real Madrid kwa kitita cha pauni milioni 42.5 hadi sasa mchezaji huyo amefanikiwa kutwaa taji la Kombe la FA tangu alipojiunga na timu hiyo.