Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA) imeendelea kutoa elimu kwa umma ikiwemo kuelimisha wananchi kuhusu kufikisha malalamiko yao wanapopata changamoto wakati wa kutumia usafiri huo.
Akizungumza na wananchi waliofika atika banda lao lililopo kwenye maonyesho hayo ya 47 ya biashara, Afisa Udhibiti Uchumi wa TCAA, Rashid Mngoya amesema TCAA imeanzisha dawati maalumu linaloshughulikia malalamiko ya mtumiaji na mtoa huduma usafiri wa anga l;inalofahamika kama CCU.
Amesema dawati la CCU lina miaka mitano tangu lianzishwe lengo ni kumlinda mtumiaji wa usafiri wa huo kama sekta zingine.
“Nitoe wito kwa wananchi hasa watumiaji wa usafiri anga kuhakikisha wanapopata shida wawasiliane TCAA dawati la malalamiko ili waweze kushughulikiwa na watanzania wengi hawa uelewa na elimu juu ya dawati hilo wamekuwa wakipitia changamoto nyingi,” amesema Mngoya.
Amesema uwepo wa CCU ni takwa la Mamlaka ya usafiri wa anga Duniani ili kuhakikisha mtumiaji wa usafiri huo wanapata stahiki zake zote kwa mujibu wa Sheria
Aidha, amesema kwa mwaka wanapokea kesi zaidi ya kesi 20 nyingi ni za kuachwa na ndege wakati wa kusafiri, kuchelewesha na kupotea kwa mzigo.