WAZEE wa Jiji la Tanga wametakiwa kuwasihi madiwani kuondoa tofauti zao badala yake wajitafakari ili kuona uchungu wa maendeleo ya wananchi ambao waliwapa ridhaa wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana ili kumaliza mgogoro wa nafasi ya meya uliopo hivi sasa.
Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella juzi wakati akizungumza na wazee wa Manispaa ya Tanga kwa lengo la kujitambulisha kwao baada ya kuteuliwa na Rais Dk. John Magufuli kushika wadhifa huo.
Hatua hiyo inatokana na kuwapo mvutano wa nafasi ya umeya ambapo vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vinapinga mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mustapha Selebosi kutangazwa mshindi.
Selebosi alitangazwa kushika wadhifa huo, Desemba mwaka jana, kitendo kilichosababisha kuibuka vurugu kubwa.
Vurugu hizo zilitokea kwa kile kinachodaiwa kuwa CCM haikuwa na idadi kubwa ya wajumbe ya kuwapatia ushindi.
“Jambo hili tunapaswa kushirikiana pamoja ili kupatikana ufumbuzi haraka, tunakwenda kwenye bajeti kuu ya Serikali, Baraza la Madiwani halijakaa na kujadili, tuwe na dhamira moja ya kujadili matatizo ya wananchi.
“Tungekuwa na uchungu wa jiji letu kama madiwani tungekaa na kujadili bajeti na kuipitisha, hili nalo limeshindwa kufanyika, niwasihi wazee wetu tukae na pande mbili zinazovutana ili tumalize mgogoro huu,” alisema Shigella.
Aliwataka pia wazee hao kuwafichua watu wanaoendelea kulipwa mshahara na Serikali wakati muda wao wa utumishi serikalini umekwisha.