Na Clara Matimo, Mwanza
JUMLA ya Wanawake na vijana 140,604 katika wilaya za Buchosa, Sengerema na Ilemela mkoani Mwanza watanufaika na uwezeshaji wa kilimo cha viazi vitamu na lishe ili kutokomeza utapiamlo, kuboresha makazi na kuwezeshwa kiuchumi waweze kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha.
Wananchi hao ambao ni Wanawake 56,000, wanaume 42,500 na vijana wa kiume na kike wa kuanzia miaka 18-35 wapatao 5,840 watanufaika kupitia mradi wa miaka mitano wa ‘Tufunguke’ unaotekelezwa na taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha kuboresha uchumi wa nyumbani (Tahea) kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la WE EFFECT la nchini Sweden lenye Makao yake jijini Nairobi nchini Kenya ukigharimu Sh milioni 792.4, ambapo pamoja na mambo mengine jamii katika maeneo hayo itawezeshwa kumiliki ardhi na kuwa na makazi bora.
Mkurugenzi wa Tahea, Mary Kabati akizungumza na Mtanzania Digital Juzi amesema lengo la mradi huo ambao ulianza Januari mwaka huu unaotarajia kuisha Desemba, 2027 ni kumuwezesha mwanamke kumiliki makazi bora hivyo wameona ni muhimu kuanza kumuunganisha na fursa mbalimbali zitakazomuinua kiuchumi ili aweze kufikia adhima hiyo.
“Zao la viazi linampa nguvu mwanamke kwa sababu akilima kisha akavuna anakuwa na maamuzi juu ya matumizi ya viazi alivyovuna hivyo anaweza akauza na kutumia pesa alizopata kuboresha makazi, lakini pia zao hilo linamhakikishia usalama wa chakula katika familia yake kw sababu anaweza kuvitumia kwa milo mitatu asubuhi, mchana na hata jioni,” amesema Mary.
Afisa Miradi wa Tahea, Mussa Masongo amesema wanataka kuboresha makazi ya wananchi hao, chakula katika kaya na kuwainua wanawake na vijana ambao hawajafikiwa na huduma sahihi ili kuisaidia serikali kusukuma gurudumu ifikapo 2030 jamii hasa ya wanawake na vijana waweze kukopesheka kwa kumiliki ardhi na kufanya shughuli za uzalishaji uchumi.
“Endapo watashiriki katika shughuli za uzalishaji mali wataweza kuboresha vyoo, mazingira yao, kuweka maji na umeme, na kufikia usawa wa kijinsia katika kuamua rasilimali kwenye kaya zetu na kufanya maamuzi sahihi juu ya mwili wake na masuala ya kifamilia. Lengo letu ni kuwafanya vijana wa aina zote kushiriki katika shughuli za uchumi ili tunaposema Tanzania isiyokuwa na umasikini inawezekana,” amesema Masongo.
Kwa upande wake, Afisa Mradi wa ‘Tumefunguka’, Bundala Ramadhani, alisema wanawawezesha akina mama kuzalisha chakula kwa zao la viazi vitatu na lishe ili kupunguza athari za utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano na usalama wa chakula kwenye kaya zao kwa sababu mama ni mkombozi kwenye familia.
Alisema akina mama hao watafundishwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi, kuelimishwa namna ya kuzalisha shambani, kutambua namna ya kusindika na kuuza kwa kufahamu viazi vitakavyopelekwa sokoni vina sifa gani, huku vijana ambao ndiyo wanakaya wa kesho na walezi wa watoto ni nguvu kazi ambayo itakuwa imefikiwa.
“Tunaendesha miradi yetu kwa kutumia vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana ambavyo vimesajiliwa na vina katiba zao, kazi yetu ni kuwakuza tunawabadilisha kutoka kikundi cha hisa ya kawaida wanaingia kwenye ushirika wenye lengo la kuboresha nyumba na makazi, ushirika ambao tunaamini kesho au siku za usoni watakuwa wamekuwa na wataweza kukopesheka na taasisi za kifedha ili kutimiza malengo yao.
“Ambapo watapanua wigo kwa kujenga nyumba mpya, kufanya miradi ya pamoja ya kikundi wanaweza kupewa haki na kupata unafuu wa kuendeleza makazi yao. Tutaanza Buchosa kwa kupeleka mbegu za viazi kwa ajili ya vikundi vitano vya kuanzia ambavyo kila kimoja kitakuwa na wanachama 30, lengo ni kuwapa mbegu bora kwahiyo zitakuwa aina za lishe kisha mafunzo yatafuata kwa ajili ya kuzalisha,” amesema Ramadhani.
Nao baadhi ya wanufaika wa mradi huo akiwemo, Anisia Samwel na Vumilia Mashauri wakazi wa Kata ya Kazunzu Halmashari ya Buchosa Wilaya ya Sengetema m
koani Mwanza wameishukuru Tahea kwa kuwapelekea mradi huo kwani familia zao na jamii inayowazunguka zitanufaika kwa kupata lishe bora, elimu jinsi ya kulima zao hilo kwa tija , kusindika na kutengeneza vitafunwa mbalimbali.
Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Buchosa Nestory Mjojo ametoa wito kwa wakulima kufuata na kuzingatia hatua zote za kilimo bora kwa zao la viazi vitamu walizowafundisha pamoja na uongezaji thamani waliyopatiwa na Tahea ili walime zao hilo kwa tija na waweze kunufaika.