Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amesema hakuna ukweli wowote juu ya muda wa miaka 100 wa uwekezaji kwenye Bandari ya Dar es Salaam kupitia Kampuni ya DP World kutoka Falme za Kiarabu kama inavyoenezwa.
Itakumbukwa kwamba kwa siku kadhaa sasa kumekuwa na maneno mengi hususan katika mitandao ya kijamii juu ya uwepo wa mkataba wa kampuni hiyo kutaka kuwekeza bandarini kwa miaka 100 – jambo ambalo limezua taharuki.
Akizungumza kutoka nchini Italia kwa njia ya Mtandao wa Youtube mapema leo Mcha a Juni 7, kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani ambaye pia ni mbobezi wa masuala ya sheria amesema yeye kwa maoni yake binafsi hajaona mahala panapoonyesha kampuni hiyo kupewa ofa ya miaka 100.
“Wakati huu ambao Chadema itatoa taarifa kuhusiana na sakata hili, mimi kwa maoni yangu binafsi nasema kuwa sijaona mahali popote kunapoonyesha kuwa Kampuni ya DP World wamepewa ofa ya miaka 100 ya kuendesha Bandari yetu,” alisema Lissu.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini Tanzania (TPA), jana uni 6, 2023 walilazimika kutoa taarifa kwa Umma, juu ya uwapo wa kikundi cha watu walioamua kwa makusudi kupotosha kuhusiana na mchakato wa maboresho ya Bandari nchini yenye lengo la kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Sehemu ya taarifa hiyo ya TPA ilibainisha kuwa: Taarifa sahihi ni kuwa Azimio la Bunge linahusu Makataba ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaingia na Serikali ya Dubai wenye ukomo wa miezi 12kwa ajili ya kutoa nafasi kwa Serikali ya Tanzania kujadiliana na Serikali ya Dubai kuhusu maeneo ambayo Serikali hizo mbili zinaweza kushirikiana katika uboreshaji wa Sekta ya Bandari nchini Tanzania,” ilieleza taarifa hiyo ya TPA.