26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mwenge wa Uhuru kuzindua miradi 99 ya Trilioni 4.4 Pwani

Na Gustafu Haule, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge,amesema kuwa Mwenge wa Uhuru ulioingia leo Mkoani kwake utaweka mawe ya msingi, kuzindua na kufungua jumla ya miradi 99 ya maendeleo yenye thamani ya Sh.trilioni 4.4.

Kunenge ameyasema hayo leo Mei 15, wakati akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa  Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa, katika eneo la Ubena katika  Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.

Kunenge amesema Mwenge wa uhuru utakimbizwa zaidi ya kilomita 1000 kukagua miradi mbalimbali katika Wilaya saba na Halmashauri tisa za Mkoa wa Pwani ambapo kati ya miradi hiyo 99, tisa itafunguliwa, 15 itazinduliwa,20 itawekewa mawe ya msingi na 55 itakaguliwa.

Ameongeza kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 yenye kauli mbiu: “Tunza mazingira, okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa viumbe hai” itasaidia kulinda na kutunza mazingira na kuufanya mkoa huo kuendelea kuwa wa kijani.

“Katika kuunga mkono jitihada za Serikali kutunza mazingira hadi kufikia mwezi Aprili mwaka 2023 Mkoa wa Pwani umepanda miti milioni saba sawa na asilimia 57.5 katika maeneo mbalimbali na  lengo letu ni kupanda miti milioni 13 kwa mwaka huu,” amesema Kunenge.

Kunenge amesema hatua hiyo inalenga uboreshaji wa mazingira na kutekeleza matakwa ya sheria ya mazingira ya mwaka 2004 ambayo yanataka shughuli zote zinazofanyika zizingatie tathmini ya athari za mazingira.

Aidha, Kunenge amesema tayari mikakati mbalimbali ya utunzaji mazingira imefanyika ikiwemo kufanya doria  kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji vinavyotokana na shughuli za kibinadamu,  kilimo, ufugaji na uchomaji miti hovyo, uhamasishaji na utoaji wa elimu juu ya umuhimu wa kutunza mazingira na kuzindua kampeni ya matumizi ya nishati mbadala ambayo yatazalisha fursa nyingi za kiuchumi.

Mbio za Mwenge wa uhuru mwaka 2023 zinakimbizwa na timu ya watu sita wakiongozwa  na Abdallah Shaibu Kaim na unatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 14, mwaka huu mkoani Manyara.

Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdallah Shaibu ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Morogoro kwa ushirikiano mkubwa pindi wakiwa Mkoani humo huku akiamini hata kwa viongozi wa Mkoa wa Pwani watatoa ushirikiano huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles