24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyabiashara Kariakoo bado ‘ngoma mbichi’

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

WAFANYABIASHARA wa Kariakoo wamegoma kufungua maduka yao kwa muda usiojulikana mpaka hapo Serikali itakapoamua kutatua kero zao zote wamechoka huku wanaomba kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Itakumbukwa kuwa siku tatu zilizopita Uongozi wa wafanyabishara hao ulifanya kikao na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla kwa lengo la kujadili namna bora ya kutatua changamoto zinazowakabili.

Mapema leo Jumatatu Mei 15, akizungumza katika mgomo huo ulioanza leo mbele ya viongozi mbalimbali wa Serikali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Martin Mbwana amesema changamoto kubwa zinazowakabili ni tatu.

Mbwana amezitaja changamoto hizo kuwa ni kamata kamata inayofanywa na Maafisa wa TRA, Usajili wa Stoo kutaka ziwe wazi na kujulikana mzigo unaoingia na kutoka na uwazi na usawa Bandarini upande wa Forodha huku pia wakilalamikia ushuru mkubwa wa vitenge.

“Changamoto kubwa ni mfumo mpya wa usajili wa stoo ambazo wafanyabiashara wanahifadhia bidhaa zao na baada ya kusajili gharama inakuwa kubwa zaidi hali inayosababisha wafanyabiashara kupata hasara,” amesema Mbwana.

Mbwana ametaja changamoto nyingine kuwa ni pindi wateja wao kutoka nchi za Kongo au Visiwa vya Comoro wanapokuja nchini kununua mzigo na risiti wanapewa lakini wanapofika njiani wanakamatwa na kwamba wanashindwa kujieleza kutokana na changamoto na hata kiswahili hawajui.

“Kitendo hiki cha kuwakamata wateja wa kigeni kinaleta usumbufu na hawawezi kurudi tena Tanzania kuja kununua bidhaa kutokana na usumbufu huu wanaoupata, kinachotokea wanapotea na Karikoo inakuwa kama shamba la bibi na baadhi ya wafanyabiashara wamehama kufanya biashara Kariakoo,” amesema Mbwana.

Amesema msimamo huo wa wafanyabiashara wa kutofungua maduka ni msimamo wa wafanyabiashara wote mpaka hapo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan atakapowasikiliza.

Amesema imekuwa ni kawaida kwa wafanyabiashara hao wanapogoma viongozi hufika na kuwataka wafungue maduka baada ya wiki mbili hali inarudi kama zamani hakuna mabadiliko wanayoyaoona.

Makalla asema hadi Mei 17…

Nae, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla akizungumza na wafanyabishara wakati mgomo huo ukiendelea amepiga marufuku kamata kamata zote ikiwemo ile inayofanywa na Maafisa TRA kukamata wafanyabiashara kuanzia leo huku akishauri wafanyabishara hao kufungua maduka yao jambo ambalo limepingwa na wafanyabiashara hao.

Amesema amesikiliza changamoto zote na kuahidi kuzifanyia kazi itakapofika Mei 17, ambapo watakaa kikao na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Ashantu Kijaji na Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata na Kamati ya Wafanyabiashara itakayoundwa leo ili kujadili kwa kina changamoto hizo.

“Naelewa umuhimu wa soko la Kariakoo, watu wengi hutegemea soko hili ikiwemo machinga hakuna haja ya kufunga maduka na changamoto hatuwezi kukimbia kuendelea kugoma hatupati suluhisho subirini mazungumzo yatakayofanyika.

“Sina pingamizi na watakaofungua biashara na wasiofungua ila ni vyema kuwa watulivu wakati viongozi wao wakiendelea kuyafanyia mazungumzo kati wafanyabiashara na serikali amewaomba kuipima imani serikali katika hili,” amesema Makalla.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao bado hawajafungua maduka hayo.

Wakati huohuo taarifa iliyotolewa na Serikali kwa umma imebainisha kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajia kuonana na kamati ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo Mawaziri wa sekta husika na TRA.

Mkutano huo unatarajiwaa kufanyika siku ya jumatano saa nane mchana kwenye ofisi ya Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo imewataka wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao za biashara wakati Serikali ikijiandaa kukutana nao kwa lengo la kuwasikiliza na kushughulikia kero zinazowakabili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles