Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wakati Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari ukiwa tayari umewasilishwa bungeni, wadau wa habari nchini wameiomba Serikali kuangalia upya baadhi ya vifungu vilivyopo kwenye muswada huo ikiwamo lugha iliyotumika.
Akizungumza katika kikao cha Wadau wa Kupata Habari (CoRI), Aprili 20, 2023, jijini Dar es Salaam Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema pamoja na kile kilichowasilishwa bungeni katika Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari, bado kuna vipengele muhimu vya sheria hiyo vimeachwa nje.
“Pamoja wanaishukuru serikali kutokana na lengo la kuifanya tasnia ya habari kuwa huru hasa kusimamia mchakato wa mabadiliko ya sheria ya tasnia hiyo. Kusudio jema la serikali tumeliona. Limefanya kile ilichofanya kwa lengo lilelile la kuboresa mazingira ya habari na wanahabari, tunashukuru katika hilo maana baadhi tumeyaona kwenye muswada.
“Lakini sheria ikibaki kama ilivyopendekezwa kwenye muswada ule, hatuwezi kufanya kazi kwa uhuru na weledi tuliokusudia. Hatususi kwa kile kilichopelekwa, tutaendelea kushawishi kuda mabadiliko ten ana tena. Mchakato wa sheria ni wa kuendelea, tukiotoka sisi watakuja wengine kuendeleza tulipoishia,” amesema Meena.
Upande wake, Rose Mwalongo, kutoka Taasisi ya Vyombo vya Vyombo kwa Maedneleo ya Jamii (TAMCOTE) amesema, angetamani kuona mapendekezo ya wadau wa habari yote yameingizwa kwenye Muswada wa Sheria ya Habari yuliwasilishwa bungeni.
“Kama mwanahabari nilitamani kuona mapendekezo yote yamepelekwa na kuwa kwenye muswada wa sheria, lakini mengi hayapo. Kuna hili la magazeti kuendelea kukata leseni kila mwaka, hili naamini linapaswa kuondolewa,” amesema Rose.
Mjumbe wa CoRI, Deus Kibamba amesema ni heshima kuwa serikali imeipa tasnia ya habari kwa kuanzisha na kusimamia mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari mpaka hapa ulipo.
Ameongeza kuwa, serikali ilikusudia kuondoa vikwazo na ndio maana Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Habari una mambo mazuri ndani yake.
“Muswada huu ambao serikali imeupeleka bungeni, una mambo mazuri lakini ni machache, mengi bado hayaingizwa. Tunaomba wabunge wajue kuwa kuna mambo mengine zaidi ya habari ambayo tumependekeza, tunaomba yaingie kwa lengo lille ile la kuimarisha tasnia ya habari,” amesema Kibamba.
TEF kuzungumza na Wabunge
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema wadau wa habari walipeleka maoni yao kwa serikali wakitaka utaratibu wa utoaji leseni kwa magazeti ufutwe kwa kuwa ni kuwaumiza wanaowekeza kwenye tasnia ya habari.
“Tutakwenda kuzungumza na wabunge juu ya athari ya baadhi ya vifungu vilivyomo kwenye sheria na marekebisho yaliyofanywa na Serikali ili watusaidie kurekebisha siku wakianza kujadili bungeni,” amesema Balile.
Balile ameongeza kuwa miongoni mwa kifungu ambacho wanataka kifanyiwe marekebisho ni cha tisa ambacho kinampa mamlaka Mkurugenzi wa Habari (Maelezo) kutoa leseni ya kuchapisha gazeti.
Amesema wanachokitaka wadau wa habari ni magazeti yapewe usajili kama ilivyokuwa zamani na si leseni kama inavyotakiwa katika sheria.
Amesema kila chombo cha habari kina leseni za biashara zinazotolewa na mamlaka za maeneo ambako biashara husika ipo hivyo hakuna sababu tena gazeti kupewa leseni na maelezo.
“Kwa mazingira yetu mtoa leseni ndiye mnyang’anyaji, hili tusingelipenda liendelee hivyo tunakwenda kufanya uzengezi kwa wabunge ili wajue athari ya jambo hili kwa biashara,” amesema Balile.
Naye Wakili James Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Misa-Tan amesema, sheria ina upungufu ambao unapaswa upigiwe kelele na ufanyiwe marekebisho ili sekta ya habari ikue zaidi.
Amesema mapendekezo ya sheria yaliyotolewa na serikali ni maeneo tisa tu kati ya 21 yaliyopendekezwa yafanyiwe marekebisho na serikali.
Amesema miongoni mwa mapendekezo yaliyofanyiwa kazi na Serikali na wanaunga mkono kifungu cha 5 (1) kwa kumuondoa Mkurugenzi wa Habari Maelezo kuwa mratibu wa matangazo kwa vyombo vya habari.
“Kifungu 38 kinachozungumzia kashfa ambavyo awali ilionekana ni jinai nacho kimefanyiwa marekebisho lakini mengi ni kupunguzwa kwa makosa na adhabu zake badala ya kuondoa,” amesema Wakili Marenga.