Na Gustafu Haule, Pwani
KATIKA kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kampuni ya Kyem General Supplies Limited ya Kibaha Mailimoja imeendelea kushirikiana na jamii ambapo hii leo Aprili 9, 2023 imewakutanisha pamoja walemavu, wajane, yatima na wazee wasiojiweza kwa ajili ya kula pamoja.
Kampuni hiyo ambayo inajishughulisha na uuzaji na usambazaji wa vyuma chakavu pamoja na vifaa vya ujenzi imeishika mkono jamii hiyo kwa kuwapa vyakula mbalimbali ikiwemo mchele, nyama na fedha .
Hafla hiyo imefanyika leo katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo Mtaa wa Mailimoja B’uliopo katika Halmashauri ya Kibaha Mjini mkoani Pwani ambapo wanufaika wake ni jamii inayoishi jirani na kampuni hiyo.
Mkurugenzi msaidizi wa kampuni hiyo, Frank Joseph, amesema kuwa kufanyika kwa tukio hilo ni utaratibu wa kampuni katika kuungana na jamii ya watu wasiojiweza.
Joseph amesema kuwa kampuni ya Kyem inatambua umuhimu wa jamii ya watu wenye mahitaji maalum na wale wasiojiweza na kwamba wanachofanya ni kurudisha asilimia ya faida wanayoipata kwa jamii.
Amesema mbali na kusaidia jamii hiyo lakini pia kampuni imetoa kipaumbele cha kuajiri vijana wengi wanaotoka katika Mtaa huo ili nao waweze kujikwamua kiuchumi na hivyo kutunza familia zao.
“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais mahiri Dk. Samia Suluhu Hassan inafanyakazi kubwa ya kutoa ajira kwa vijana lakini haitaweza kuwafikia wote kwa wakati mmoja lakini kampuni yetu imeamua kubeba jukumu la kusaidiana na serikali katika kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana,” amesema Joseph.
Aidha, Joseph ameongeza kuwa kampuni yake imeweka mipango mikubwa ya baadae ikiwemo ya kuajiri vijana wengi zaidi kulingana na mahitaji ya kampuni yatakavyokuwa pamoja na kuendelea kuisaidia jamii ya watu wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mailimoja B” Shauri Yombayomba , ameishukuru kampuni ya Kyem kwa namna inavyojitoa kusaidia jamii.
Yombayomba amesema kuwa awali alipata taarifa kutoka kwa uongozi wa kampuni hiyo kuhusu namna ya kusudio la kutaka kuifikia jamii hiyo kwa kula nao pamoja sikukuu na ndio aliporidhishwa na hatua hiyo.
Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo alilazimika kuratibu zoezi la kubainisha jamii ya watu wenye ulemavu,Yatima,Wajane na Wazee kwa kila balozi waliopo katika mtaa wake na hivyo kupata idadi sahihi na hatimaye kuwafikisha katika kampuni hiyo.
Baadhi ya jamii iliyonufaika na mpango huo akiwemo, Zainabu Athumani na Ally Abdallah wamesema kuwa kitendo cha kampuni hiyo kuijali jamii yenye mahitaji maaalum ni wazi kuwa imejiwekea hazina kubwa mbinguni.
Hata hivyo, wameiomba kampuni hiyo kuendelea na mpango huo hata katika siku za baadae kwakuwa inawasaidia kupunguza adha ya hupatikanaji wa chakula katika familia zao.