Na Clara Matimo, Mwanza
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imesema imeridhishwa na matumizi ya fedha yaliyotumika katika mradi wa meli mpya ya Mv Mwanza hapa kazi tu inayojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 109.
Akizungumza Machi 27, 2023 baada kutembelea na kugagua ujenzi wa meli hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jerry Silaa amesema wanaamini mwaka huu wa fedha utakapomalizika hesabu ya uwekezaji wa mitaji ya umma itaongezeka.
“Tumeona mkandarasi yupo site kazi inaendelea kwa hiyo tunaposema ile salam yetu kwamba kazi iendelee hapa tunaona kwa vitendo kwamba kazi inaendelea, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan
hakuna mradi uliosimama.
“Tumeridhika na kazi hapa tunaamini uwekezaji wa mitaji ya umma unafanyika vizuri,” amesema Silaa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Meja Jen. John Mbungo amesema watahakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika nao.
“Tunafurahi sana kamati PIC imekuja kujionea namna ambavyo miradi ya kimkakati inavyoendelea wameona kzi inavyoendelea, mimi kama Mwenyekiti wa bodi ni kuhakikisha bodi inakuwa na sera sahihi na bora.
“Sera zenye kuleta tija ili kazi zote zinazofanywa chini ya kampuni hii zinafanyika kwa wakati na kwa tija kubwa na kwa mafanikio makubwa zaidi,” amesema Meja Jen. Mbungo.
Meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 80 ni kubwa kuliko zote za Ukanda wa Maziwa Makuu.
Ina urefu wa mita 92.6 inakwenda juu mita 20 na upana mita 17 inauwezo wa kubeba tani 400 za mizigo na abiria 1200.