27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Sura nyingine ya Magufuli

MAGUFULI*Aanza mkakati kunasa vijana, apiga simu kwenye Tv

*Ikulu, wachambuzi wazungumzia hatua yake

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SURA nyingine ya upande wa maisha ya Rais Dk. John Magufuli katika kuliongoza Taifa imedhihirika baada ya jana asubuhi kuwashangaza Watanzania kwa uamuzi wake wa kupiga simu katika kituo cha runinga cha Clouds.

Dk. Magufuli alipiga simu wakati wa kipindi cha Clouds 360 kueleza kufurahishwa kwake na kipindi hicho, ikiwa ni mara ya kwanza kufanya mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha habari nchini tangu alipoingia madarakani Novemba 5, mwaka jana.

“Mimi nawapongeza sana kwa kweli,” alisema Dk. Magufuli kabla ya kuendelea na kutaja majina ya watangazaji wa kipindi hicho na kusema huwa wanachambua vyema magazeti.

Katika mazungumzo yake katika kipindi hicho, Rais Magufuli alikuwa akiwataja kwa majina watangazaji Hudson Kamoga, Samuel Sasari na Baby Kabaya ambao aliwapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya, ikiwa ni pamoja na namna walivyochambua magazeti na mijadala mingine, ukiwamo ule wa ziara yake aliyoifanya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Machi 10, mwaka huu.

Pamoja na hali hiyo, Rais Magufuli aliisifu Clouds Media Group kwa namna wanavyofanya kazi, huku akigusia tukio la ‘Malkia wa Nguvu’ lililolenga kutambua mchango wa wanawake nchini katika kuzitambua fursa na kuzifanyia kazi ipasavyo.

 

MAHOJIANO YALIKUWA HIVI

Rais Magufuli: Nawapongeza sana, bahati nzuri nimeshika majina yenu, wewe ni Hudson, mwingine Baby, mwingine anaitwa Sam, mnapozungumzaga mnapokuja kuanza magazeti yenu kuna aina yake ya tofauti, nimeamua kuwapigia kuwapongeza.

Mimi ni shabiki wenu mzuri kweli, lakini bahati nzuri nyie wote wazuri, kwahiyo Sam unanifurahishaga usione na huyo Baby.

Hudson: Kuna jambo moja tunataka kukuuliza, tulikuwa na kampeni kuwajuza Watanzania kuhusu fursa 10 ambazo wakizitumia wanaweza wakafika mbali sana kama nchi, tunaweza kuisaidia Serikali kupiga hatua ya kiuchumi na maendeleo.

Nilikuwa naangalia sasa fursa 10 nyinyi mlizotoa kwa wanawake tu, wanaume hamkuwapa zawadi, nafikiri kwa sababu ya mwanamke tukimuwezesha na kuelekea 50/50 uwakilishi tunaweza kufikia.

Magufuli: Basi mimi nawapongeza, huyu hapa mke wangu ongeeni nae na yeye.

Hudson: Malkia wa nguvu Janeth Magufuli, shikamoo mama.

Janeth: Marhaba, tumefurahi kuzungumza na wewe, yaani na sisi uwa tunafurahi tunawashabikia sana.

Watangazaji: Asante sana mama.

Janeth: Ahsanteni jamani, yaani mnatupa faraja, huwa tunacheka sana na mume wangu hapa, mbarikiwe sana, tunawapenda sana, haya huyu hapa mzee ongeeni nae.

Magufuli: Sasa siku nyingine mje mtangaze na wake zenu hapo, Baby aje na mume wake, Hudson aje na mke wake hapo tuwaone.

Hudson: Asante, tunakutakia kazi njema uongozi mwema.

 

MJADALA BAADA YA KUKATA SIMU

Hudson: Nilivyoona simu, nikaangalia hizi namba, sauti, nikasema mmmh! Nimuulize huyu nani ama niendelee, nikasema nikiuliza nani atasema hili nalo jipu, ananiulizaje nani, Magufuli atakuwa mtazamaji namba moja wa 360 na mama atakuwa namba mbili.

Baby: Tumefurahi familia yote inayoangalia 360, yaani nilitoka jasho nikasema inakuwaje, lakini kuna wazo rais ametoa kuja na wake zenu, mtihani huu.

 

AFUATA NYAYO ZA MUSEVENI

Hatua hiyo ya Rais Magufuli inatanguliwa na ile ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ambaye naye huwa na utamaduni wa kupiga simu moja kwa moja studio wakati wa vipindi vya moja kwa moja vikiendelea redioni.

Katika moja ya tukio kubwa linalokumbukwa na Waganda wengi, ni hatua ya rais huyo kupiga simu kituo kimojawapo cha nchini Uganda, kilichokuwa kikirusha kipindi ambapo wasilikilizaji walikuwa wakiikosoa familia yake na yeye mwenyewe.

Akiwa katika msafara wake wa safari za ndani nchini humo, alisimama na kupiga simu moja kwa moja na kuwataka watu waache kuishambulia familia yake.

Mbali na hali hiyo, pia alikuwa akiandika makala na barua kwenye magazeti na alikuwa anajadiliana na wasomaji waliotoa maoni kwa kujibu hoja zao.

 

KWANINI MAGUFULI AMEAMUA KUPIGA SIMU CLOUDS TV

Clouds Media Group inamiliki vituo viwili vya redio na kituo cha runinga ambapo ni moja ya vituo vinavyoongoza kwa kuwa na wasikilizaji na watazamaji vijana.

Inaelezwa kuwa huenda hatua ya Rais Magufuli kupiga simu Clouds Tv ni mkakati wake wa kuwafikia vijana kwa njia rahisi.

 

KAULI YA IKULU

MTANZANIA ilipomtafuta Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa kuzungumzia hatua hiyo ya Rais Magufuli kupiga simu katika kipindi cha televisheni kilichokuwa ‘live’, alisema inaonyesha ni namna gani kiongozi huyo wa nchi alivyo na ukaribu na Watanzania waliomchagua.

“Ni tukio ambalo Mheshimiwa Rais Magufuli amelifanya yeye mwenyewe akiwa na mke wake mama Janeth, kwahiyo hatua hii ni wazi unaona namna ukaribu uliopo kwa kiongozi wetu wa nchi.

“Rais Magufuli ni Mtanzania kama ulivyo wewe (mwandishi), anayo haki kama raia mwingine ya kutoa maoni yake kuhusu jambo fulani.

“Hatua hii inaonyesha nia njema ya Rais Magufuli, hasa katika kuwa kwake karibu na sekta ya habari na mapenzi kwa vyombo vyote vya TV, redio na magazeti yetu nchini,” alisema Msigwa.

 

  1. RIOBA

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), Dk. Ayub Rioba akitoa maoni yake kuhusu hatua hiyo Rais Magufulia,  alisema kuwa ni jambo la kawaida na si la kushtua wala kushangaza kwani kiongozi huyo amekuwa akipenda kuwa karibu sana na wananchi

“Pia ni mfuatiliaji wa mambo yanayoendelea sehemu mbalimbali nchini, hivyo kupiga simu katika kituo hicho ni kitendo cha kawaida na ni haki yake ya msingi kama mwananchi,” alisema Dk. Rioba.

Aliongeza kuwa hata kabla ya kuwa rais, miaka 20 ya uwaziri wake alikuwa mfuatiliaji wa mambo kwa ukaribu zaidi na kwa njia za kawaida, hivyo kitendo alichofanya ni cha kawaida tu kwake.

“Sioni kama ni kitendo cha kushtua zaidi, labda cha ajabu ni ile hatua ya kutoka Ikulu kwenda Hazina, ile inashtua kuliko kupiga simu ambayo amefanya kama mwananchi wa kawaida anayefuatilia vipindi vya kawaida katika runinga,” alisema Dk. Rioba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles