Na Ashura Kazinja, Morogoro
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Daniel Chongolo amesema ipo haja ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kutembelea na kutatua mgogoro wa mradi wa umwagiliaji wa Luhindo mkoani Morogoro wenye thamani ya Sh milioni 900.1 ambao licha ya kukamilika miaka mitatu iliyopita bado haujaanza kufanya kazi.
Chongolo amesema hayo leo Jauniri 29, 2023 wilayani Mvomero mkoani Morogoro katika ziara yake ya siku tisa iliyoanza leo ambapo amesema haiwezekani Serikali ikatoa fedha nyingi katika kukamilisha miradi ya maendeleo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi huku bado mradi usifanye kazi na kuondoa maana aliyoitaka Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo nchini.
Aidha, amewataka viongozi wote wa serikali kuanzia ngazi ya vijiji kuzingatia miiko ya uongozi ili kukabiliana na migogoro ya ardhi inayoendelea kuchipua katika baadhi ya maeneo nchini.
Akizungumzia changamoto ya umeme wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa vijiji 60 ameagiza Mkandarasi kampuni ya HNXJDL INT Constructers kuhakikisha wanafika angalau asilimia 80 ya ujenzi ifikapo Februari, mwaka huu au kukamilisha ujenzi huo vinginevyo atasimamishwa kuendelea na ujenzi huo kupisha wakandarasi wengine.
Hata hivyo, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Dk. Philiphine Titus kutengeneza mpango mkakati utakaoonesha gharama halisi za ujenzi na umuhimu ili kuona haja ya kuanza ujenzi wa soko la mpunga katika wilaya hiyo.
Awali, Mbunge wa Mvomero, Jonas Van Zeeland alimshkuru Rais Dk. Samia kwa kuwasaidia katika kutatua changamoto mbalimbali kwenye wilaya hiyo licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa zinazowakabili wananchi wa wilaya hiyo.
Amezitaja changamoto zinazowakabili eneo la Dakawa kuwa ni pamoja na upatikanaji wa maji ya Bomba, kukamilika kwa Zahanati ya Kijiji na migogoro ya mipaka baina ya vijiji na vijiji
Akiwa katika shina namba 18 kwenye Kijiji hicho amepokea jumla ya wanachama 13 wapya waliojiunga na CCM.