Na Tunu Nassoro, Dar es Salaam
HALMASHAURI ya jiji la Dar es Salaam imetangaza rasmi tarehe ya uchaguzi wa meya wa jiji hilo Machi 22 mwaka huu.
Uchaguzi huo utafanyika baada ya kuahirishwa mara nne kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni mizengwe ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwazuia wapinzani kushika nafasi hiyo kwa kutumia mbinu chafu.
Inadaiwa mizengwe na mbinu hizo chafu ni pamoja na zuio batili ambalo CCM ilidai lilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Baadaye Mahakama hiyo ililikana zuio hilo.
Awali, uchaguzi huo ulikuwa ukiahirishwa kutokana na mvutano kuhusu wajumbe halali wenye sifa za kushiriki upigaji kura.
Ilidaiwa kuwa CCM kilihusisha wabunge kutoka nje ya Dar es Salaam jambo ambalo lilizua mvutano mkubwa na kusababisha uchaguzi huo kuahirishwa na kupangwa kufanyika Januari 23, mwaka huu.
Mvutano mwingine ulizuka Februari 8, mwaka huu, baada ya madiwani kufika viwanja vya Karimjee kwa ajili ya uchaguzi na kukabidhiwa barua ambazo hazikueleza sababu za kuahirishwa kwake wala tarehe nyingine ya uchaguzi.
Akithibitisha kupokea barua ya mwaliko kuhusu uchaguzi huo wa Machi 22,kutoka Ofisi za Jiji la Dar es Salaam, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob alisema ni kweli madiwani wamepokea barua za mwaliko wa uchaguzi huo.
Ofisa Uhusiano wa Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe aliithibitishia MTANZANIA kwamba maandalizi ya uchaguzi huo yamekamilika na utafanyika tarehe iliyopangwa.
“Muda huu niko Morogoro, lakini taarifa nilizo nazo ni kweli uchaguzi utafanyika Machi 22 na tayari madiwani wamekwisha kusambaziwa barua za mialiko,” alisema Makwembe.
Diwani wa Kata ya Vijibweni, Isaya Mwita (Chadema) ndiye atapeperusha bendera ya Ukawa huku mgombea wa nafasi ya Naibu Meya akitarajiwa kutoka CUF. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitawakilishwa na Diwani wa Kinondoni, Yusuph Omary Yenga.
Inaelezwa kuwa Ukawa wanapewa nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho kutokana na kuwa na idadi kubwa ya madiwani kwa vile wanaizidi CCM kwa madiwani 13.
Ikiwa Ukawa watafanikiwa kutwaa nafasi hiyo itakuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa wapinzani kuliongoza jiji la Dar es Salaam tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.