32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Nyumba ya Mkuu wa Polisi Z’bar yalipuliwa kwa bomu

hamdan-omar-makameNA SARAH MOSSI, ZANZIBAR

WATU wasiojulikana wameishambulia kwa bomu nyumba anayoishi Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame, iliyopo Kijichi mjini Unguja.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,  Kamishna Hamdani alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5.00 usiku wakati familia yake ikiwa imelala.

Alisema mlipuko huo uliharibu vibaya sehemu ya paa la nyumba hiyo pamoja na dari lake na kusababisha majeraha kwa baadhi ya watu waliokuwamo ndani.

Kamishna Hamdani alisema majeruhi hao wakiwamo watoto wake walipatiwa matibabu haraka.

“Ilipofika saa 5.00 usiku tulisikia kishindo kikubwa na tukaona moto, na baadaye tukaona paa linaanguka lenyewe,” alisema.

Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha  mlipuko uliotumiwa kuharibu nyumba yake unafanana na uliotokea hivi karibuni kwenye Maskani ya CCM Kisonge.

Hata hivyo, alisema ni mapema kuzungumza lolote kwa vile uchunguzi wa  sayansi kuhusu mlipuko huo unaendelea.

Kutokana na kushamiri kwa matukio ya kulipuliwa mabonu katika maeneo mbalimbali kisiwani Unguja na Pemba, Kamishna Hamdani alisema polisi wamelazimika kuomba msaada na kuongeza nguvu kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na vikosi vya ulinzi Zanzibar.

Alisema pia Jeshi la Polisi Zanzibar linawashikilia watu 31 kwa mahojiano   huko Pemba kuhusu matukio mbalimbali,   ikiwa ni pamoja na uchomaji wa maskani za CCM na nyumba za kuishi wananchi.

Kamishna Hamdani aliwataka wananchi kutokuwa na hofu wanapowaona mara kwa mara askari wa vikosi vya ulinzi katika maeneo wanayoishi.

Alisitiza kuwa hiyo ni sehemu ya juhudi za kupambana na matukio ya uhalifu yanayopangwa na vikundi maalumu, yakilenga zaidi siasa na kuwafanya wananchi washindwe kujitokeza kupiga kura Machi 20.

“Wapo watu au kikundi cha watu wachache wanalazimisha Zanzibar kuingia katika vurugu za siasa ili amani ipotee na baadaye waje kulilaumu Jeshi la Polisi kwamba limeshindwa kudhibiti fujo za aina hiyo,” alisema.

Kamishna Hamdani alisema Jeshi la Polisi halitakubali kuona kikundi cha watu wachache wanatumia fursa hiyo kuvuruga amani iliyopo.

Alisema ulinzi utaimarishwa katika mitaa ya mji wa Unguja na vituo vya kupiga kura   siku ya uchaguzi wa marudio, na kujihadhari zaidi siku ya kutangazwa  matokeo ya uchaguzi huo.

 

PEMBA WAKIMBILIA MOMBASA

Wakati huohuo, taarifa kutoka Pemba ambako mwandishi wetu amepiga kambi, zinaeleza kwamba baadhi ya wananchi kisiwani humo wameanza kukimbilia Shimoni Mombasa nchini Kenya wakihofia machafuko wakati wa uchaguzi huo wa marudio.

Habari za uhakika zinaeleza kwamba tukio hilo linahusisha vijana wa maeneo ya Konde na Micheweni ambao inadaiwa wengi ni wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF).

“Hapa hali inaonekana si nzuri baada ya wanajeshi na polisi kuwa wengi na wengi wao wanatoka nje ya Kisiwa cha Pemba.

“Hii hali hatujaizoea ndiyo maana tumeanza kukimbia, tunahofia kupigwa,” alisema mwananchi mmoja mkazi wa Konde aliyekataa kutajwa gazetini.

Naye mkazi wa Micheweni ambaye pia hakutaka jina lake kutajwa, aliiambia MTANZANIA kuwa usiku hushuhudia vijana wengi wakiwa wamejazana kwenye boti za kienyeji (vidau) wakielekea Shimoni, safari aliyosema inachukua saa  tatu.

“Kutoka hapa Micheweni hadi Shimoni ni safari ya muda mfupi tu, na vijana wengi ukiwauliza watakwambia wanafikiri hawako salama katika uchaguzi unaokuja, ni heri wakajisalimishe,” alisema mwananchi huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir Ali, alipoulizwa na MTANZANIA juu ya hali ya usalama katika mkoa wake, alisema hadi sasa hali ni shwari isipokuwa yapo matukio madogo aliyosema yamedhibitiwa.

Kamanda Nassir alisema polisi wameweza kupambana na matukio ya kuchomwa moto ofisi za vyama na Serikali.

Alisisitiza kuwa usalama wa wananchi umeimarishwa kisiwani humo ili waweze kupiga kura kwa amani.

Alipoulizwa kuhusu hofu waliyonayo wananchi hadi kuanza kukimbilia Shimoni, Kamanda Nassir alisema taarifa alizonazo ni kwamba wafuasi wa CUF wanakimbia kwa vile wamegoma kupiga kura kwenye uchaguzi wa marudio.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles