STOCKHOLM, SWIDENI
ALIYEKUWA nyota wa klabu ya Gor Mahia, Michael Olunga, amekuwa gumzo katika klabu yake mpya ya IF Djurgarden ya nchini Sweden, baada ya kufunga bao lake la pili mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Pelle Olsson, amesema kwamba, mchezaji huyo amekamilika kuweza kucheza soka popote duniani kutokana na uwezo wake.
“Kwanza umbo lake linambeba, lakini uwezo wake ni mkubwa na ameweza kuendana na mfumo wa timu kwa kipindi kifupi amekuwa tofauti na wachezaji wengine ambao wamekuwa wakisajiliwa.
“Hata kwa upande wa mashabiki nao wamekubaliana na uwezo wa mchezaji huyo kwa kuwa hadi sasa amefanikiwa kufunga mabao mawili kwa kipindi kifupi tangu asajiliwe, ninaamini atakuwa na mchango mkubwa sana katika timu,” alisema Olsson.
Olunga alifunga bao katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo dhidi ya Elfsborg, lakini bao hilo halikutosha kwani ulimalizika kwa sare ya 2-2.