Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMATI za Kudumu za Bunge, leo zinatarajiwa kuanza vikao vyake jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Bunge mjini Dar es Salaam jana, ilisema wabunge wote wanapaswa wawe wamewasili Dar es Salaam kuanzia jana.
“Wakati wa vikao vya kamati, jukumu la msingi litakuwa ni majadiliano ngazi ya Kamati za Bunge na Serikali kuhusu maudhui ya mpango wa mwaka wa maendeleo ya Taifa na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2016/17.
“Ratiba ya majukumu ya kamati hizi, yatatekelezwa kwa utaratibu, Machi 14 hadi 27, 2016 kamati zitakuwa na vikao kwa ajili ya kujadili taarifa mbalimbali za Serikali.
“Kila kamati itakutana na viongozi na watendaji wa Serikali kutoka katika wizara au taasisi inayoisimamiwa na kamati husika,”ilisema taarifa hiyo.
“Machi 29, kamati zote za Bunge zitapokea dondoo na randama za vitabu vya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 na kuanzia Machi 30, mwaka huu wabunge wote watapokea mapendekezo ya Serikali kuhusu Mpango wa Maendeleo ya Taifa na kiwango cha ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo, ilisema kuanzia Machi 31,mwaka huu hadi Aprili 6, Kamati ya Bajeti itachambua mapendekezo ya mpango na kiwango cha ukomo wa bajeti.