Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
WADAU wa habari nchini, hawajaonja ladha ya mafanikio ya harakati zao katika kuhakikisha, tasnia ya habari inakuwa huru na wanahabari kufurahia kazi yao.
Licha ya baadhi ya vyombo vya habari kufunguliwa, Televisheni za mtandaoni kuwa huru na kuanza kwa mazungumzo kati ya wadau wa habari na serikali, bado sheria kandamizi zimebaki kama rejea ya chochote kinachoendelea kwenye tasnia ya habari leo.
Kumekuwa na safari ndefu ya kubadilisha mazingira ya tasnia ya habari yaliyoharibika mwaka 2016, baada ya kuunda sheria mpya iliyopoka uhuru wa habaria na wanahabari.
Mwaka 2016, ndio mwaka tasnia ya habari nchini ilitumbukia katika shimo la hofu, waandishi na wafanyabaishara kupitia vyombio vya habari walianza kupoteza mwelekeo. Ni baada ya Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 kusainiwa na kuanza kufanya kazi.
Ndio wakati tasnia ya habari ilianza kusinyaa, heshima ya vyombo vya habari ikapotea huku habari za udaku, umbea na mitandao ya kina Mange Kimambi, Kigogo ikawa mbadala.
Mtamaini yamerejea, licha ya kutokuwepo mabadiliko yoyote katika sheria iliyoiingiza kichakani tasnia ya habari, angau serikali ya awamu ya sita imeona tatizo, imeanza kulishughulikia.
Kwa sasa, kama kuna jambo ambalo wanahabari nchini wanalisubiri kwa hamu kubwa, kama kuona ahadi ya Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inatimia.
Ni kuhusu kuwasilisha mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari bungeni, kama yalivyochakatwa na wadau wa habari pamoja na serikali.
Kukamilika kwa mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari, kutaondoa giza tasnia ya habari na kuanza safari mpya ya uhuru na mafanikio.
Bila shaka, nguvu ya mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari nchini ilitiwa chachu na Rais Samia Suluhu Hassan. Tangu siku zake za awali katika utawala wake, alijielekeza katika kutatua malalamiko ya wananchi, taasisi na kitaaluma.
Licha ya kuwepo kwa mchakato, mazungumzo na hatua kadhaa lakini bado hofu ya wanahabari ipo pale pale, kwa kuwa sheria zilizopo hazitoi mwanya wa kukua kwa tasnia hiyo.
Wadau wa habari tunasubiri kwa hamu kubwa, kuona serikali ikihitimisha kiu ya wanahabari ya kuwafungua minyororo iliyofungwa wakati wa utungaji wa Sheria ya Habari ya Mwaka 2016.