24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kumaliza kero ya maji kata za Isanga, Buchambi wilayani Maswa

Na Samwel Mwanga, Maswa

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda amesema Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA) imepanga kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Kata za Isanga na Buchambi wilayani Maswa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda(mwenye reflector ya rangi ya orange)akikata utepe wakati kuweka jiwe la msingi katika kituo cha kuchotea maji cha Zahanati ya Isanga wilaya ya Maswa kiluchojengwa na Ruwasa.(Picha Na Samwel Mwanga)

Dk. Nawanda amesema hayo leo Septemba 13, 2022 wilayani Maswa kwa nyakati tofauti wakati wa kuweka jiwe la msingi  katika kituo cha kuchotea maji kwenye kijiji cha Isanga na kuzindua mradi wa maji wa Inenwa-Kizungu katika kijiji cha Kizungu.

Amesema adhima ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwaondolea kero wananchi wake na kwa sekta ya maji ameamua kumtua mama ndoo kichwani hasa maeneo ya vijijini kwa kutumia Ruwasa.

“Adhima ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu ni kumtua mama ndoo kichwani na ndiyo maana leo unaona Ruwasa wanavyofanya kazi kubwa ya kusambaza maji hasa maeneo ya vijijini ambao yaliyo mengi hupatikanaji wake wa maji ni mgumu sana,”amesema Dk. Nawanda.

Amesema ili kuonyesha nia nzuri ya serikali katika suala la upatikanaji wa maji safi na salama katika  maeneo ya Kata hivyo hivyo amemwagiza Meneja wa Ruwasa mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala kuhakikisha vijiji ambavyo havijapata maji katika Kata hizo vinapata maji.

“Meneja wa Ruwasa mkoa wa Simiyu hakikisha vijiji vilivyoko katika Kata ya Isanga na Buchambi ambavyo havina maji vinapata maji na hii ni kudhihirisha kuwa awamu ya sita imedhamilia kumtua mama ndoo kichwani,” ameagiza Dk. Nawanda.

Dk. Nawanda amesema ifikapo mwaka 2025 maeneo mengi ya vijijini katika mkoa huo yatakuwa yamepata huduma ya maji kutokana na kasi kubwa waliyonayo Ruwasa kwani wamekuwa wakipata fedha nyingi za kutekeleza miradi kutoka serikalini.

Naye Meneja wa Ruwasa mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariam Majala amewataka wananchi kuitunza na kuilinda miradi ya maji ambayo imekamilika na kukabidhiwa kwao kwa ajili ya uendeshaji ili waweze kunufaika nayo kwa kipindi cha sasa na vizazi vijavyo.

“Hii miradi ambayo imekamilika tunaikabidhi kwa jamii kwa ajili ya uendeshaji maana miradi ikikamilika tunaunda chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii hawa ndiyo watakuwa na jukumu la kuhakikisha mradi wa maji unakuwa endelevu na tukumbuke serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi wa miradi hii hivyo tuilinde na kuitunza,” amesema Majala.

Awali, Meneja wa Ruwasa wilaya ya Maswa, Mhandisi Lucas Madaha akitoa taarifa ya miradi hiyo amesema kuwa mradi wa Maji wa Inemwa -Kizungu umetumia gharama ya Sh milioni 469 fedha zilizotokana na Mapambano ya Ustawi wa Maendeleo dhidi ya Covid -19  na mradi wa maji wa Isanga umegharimu kiasi sh Milioni 534 kupitia mpango wa PfR (Payment for Results).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles