30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaja na mfumo wake wa manunuzi, kudhibiti maofisa wasiosajiliwa PSPTB

*Ni baada ya ule wa TANePS kuruhusu hata wasiosajiliwa kuufikia

*PSPTB kuanza msako kwa wanaofanya kazi bila kusajiliwa

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

SERIKALI iko mbioni kukamilisha mfumo mpya wa manunuzi ya umma ambapo kukamilika kwake kutarahisha taratibu za manunuzi huku pia ukidhibiti maofisa ununuzi wasio na sifa.

Hayo yamebainishwa leo Dar es Salaam Agosti 29, 2022 na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi(PSPTB), Godfred Mbanyi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari.

Mbanyi amesema kuwa mfumo wa sasa wa manunuzi(TANePS) ulikuwa ukiruhusu mtaalamu yeyote ambaye anafanya shughuli za ununuzi hata kama hajasajiliwa kuweza kuingia.

Aidha, amesema kuwa hatua hiyo ilikuwa ikisababisha madhaifu mengi ya kimanunuzi kutokea na wakati wa ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).

“Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwasasa inajenga mfumo wake mpya wa ununuzi wa umma baada ya ule wa awali wa TANePS ambao ulijengwa na watu wa nje kuwa na changamoto.

“Moja ya changamoto hizo nikwamba mfumo wa sasa ulikuwa ukiruhusu mtaalamu yeyote ambaye anafanya shughuli za ununuzi wa umma hata kama hatambuliki na bodi kuweza kuingia na kufanya shughuli za ununuzi.

“Hii ilikuwa ikisababisha madhaifu mengi ya kimanunuzi kutokea na wakati wa ukaguzi wa CAG ulikuwa ukibaini madhaifu mengi katika michakato ya manunuzi ya umma, hivyo kwa mfumo huu mtaalamu yeyote ambaye hatakuwa amesajiliwa na bodi hataweza kuingia, kwani hataweza kutoka hatua moja kwenda nyingine bila kuweka namba ya usajili wa PSPTB,” amesema Mbanyi.

Mbanyi amesema kuwa lengo la Serikali kujenga mfumo huo mpya nikutaka kurahisisha taratibu zake za manunuzi ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali iliyopo na kutoa huduma kwa wananchi.

“Ikitokea kwamba taasisi au ofisi yoyote ya serikali maofisa ununuzi wake hawajasajiliwa na PSPTB maana yake ni kwamba wakiingia kwenye mfumo na ukawakataza kuendelea tutachelewesha kutoa huduma kwa wananchi na tunaweza kukwamisha kutekelezwa au kukwamishwa kwa miradi ya serikali.

“Ndiyo sababu tunataka watu wote walioko katika kada hii wafahamu mabadiliko hayo kwamba mfumo mpya wa ununuzi unajenga na hakuna mtu atakayeruhusiwa kufanyakzi kwenye mfumo bila kusajili ili tusiweze kukwamisha miradi ya serikali hili ni jambo ambalo tunataka wahusika wote walifahamu,” amesema Mbanyi.

Aidha, katika hatua nyingine Mbanyi amesema kuwa PSPTB kuanzia Septemba 13, mwaka huu inaenda kufanya kaguzi kwenye taasisi za umma na binafsi kuangalia wataalamu wanaofanya kazi hizo kama wamesomea na wanavigezo vingine vya kitaaluma ikiwamo usajili.

“Kwani tumekuwa tukiona kwenye taarifa za ukaguzi kwamba taasisi flani imefanya manunuzi chini ya kiwango lakini manpokwenda kufanya kaguzi mnabaini kuwa hata wale wenyewe waliokuwa wanafanya kazi hizo hawajasomea na hawana sifa sitahiki.

“Kwani PSPTB ndiyo imepewa mamlaka kisheria kuainisha vigezo vya kitaaluma katika fani ya ununuzi na ugavi nchini, hii ina maana kwamba kama tutafika kwenye taasisi kwa mkuu wa kitengo cha manunuzi basi anatakiwa awe na sifa kadhaa ikiwamo kusajiliwa kwa ngazi inayotakiwa.

“Hivyo tutafanya kaguzi kwenye taasisi za Serikali na binafsi ili kuhakikisha kuwa maadili ya taaluma hii yanafuatwa, hivyo mtu atakayekutwa akifanya kazi hiyo kinyume cha sheria basi atawajibishwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Mbanyi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles