30.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau waridhishwa na mwitikio wa Serikali mabadiliko Sheria ya Habari

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika(MISA-TAN), Wakili James Marenga amesema kuwa wanaoina nia njema inayonyeshwa na Serikali katika kuelekea mabadiliko ya Sheria ya vyombo vya habari nchini.

Wakili James Marenga.

Wakiliwa Marenga ameyasema hayo mapema leo Agosti 27, 2022 kwenye kipindi cha Jicho letu ndani ya Habari kinachorushwa na kituo cha Luninga cha Star TV.

Kauli hiyo ya Wakili Marenga imekuja ikiwa ni siku moja tu tangu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kuthibitisha kuwa Serikali ipo tayari kutatu changamoto zilizopo.

“Kwa sababu lengo letu ni kutatua changamoto ambazo tunaziona kwa hiyo serikali ipo tayari, kikao cha kwanza kimeenda vizuri na kikao cha pili ambacho nitakwenda mwenyewe tukae pamoja tuzungumze tujenge hoja, wanawaza nini, tunawaza nini na mwisho tutakubaliana, nchi ni yetu wote,” alisema Waziri Nape.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Wakili Marenga amesema hadi sasa serikali imepokea na kukubali kufanyia kazi vipengele mbalimbali ambavyo wameviwasilisha kuhusu Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016.

“Tayari tumewasilisha serikalini vifungu vyenye utata kwenye sheria hii ambavyo vimekuwa ni changamoto, tunashukuru kwamba tunaiona nia njema ya serikali katika kufanyia kazi mabadiliko ya vifungu ambavyo tumeviwasilisha kwani imepokea vizuri maoni hayo ya wadau na imeahidi kuyafanyia kazi,” amesema Wakili Marenga.

Marenga amesema kuwa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 imemtambua Mwandishi wa Habari ni nani kwani awali ya hapo alikuwa hatambuliki.

“Kabla ya kuwapo kwa sheria hiyo kulikuwa na sheria ya mwaka 2006 ambayo ilikuwa na changamoto kubwa sana ya udhibiti na uchapishaji.

“Sheria hiyo ilikuwa ikimpa mamlaka makubwa sana Waziri wa Habari kudhibiti uchapishaji wa magazeti,” amesema Marenga.

Akifafanua zaidi juu ya changamoto ilipo katika sheria hiyo Wakili Marenga amesema kuwa kumekuwa na maeneo ambayo wanahabari wanaona kuna haja ya kufanyiwa kazi.

“Shida iliyopo katika sheria hii ni kwamba kumekuwa na maeneo ambayo wanahabari wameona kuna changamoto ya kuyafanyia kazi na tayari.

“Mfano eneo la kwanza ambalo lilikuwa na changamoto ilikuwa ni ofisi ya msemaji Mkuu wa Serikali ambayo imepewa mamlaka makubwa sana ya kusajili, kutoa leseni.

“Na na inasema kuwa magazeti yatakuwa yanapewa leseni kila mwaka hivyo tumezungumza na serikali imesema itaenda kulifanyia kazi, pia jambo jingine ni kwamba Mkurugenzi wa idara ya habari maelezo alipewa mamlaka ya kudhibiti matangazo, hili pia tumelizungumza na serikali imesema inaenda kulifanyia kazi.

“Awali kanuni zilikuwa zinamruhusu Mkurugenzi huyu kuangalia ni wapi atapeleka matangazo hayo baada ya kuwa ameyapokea jambo ambalo linaleta upendeleo na wasiwasi wa kupata matangazo hayo kwa vyuombo binafsi hasa ambavyo vina mrengo tofauti.

“Eneo jingine ni utoaji wa taarifa ambapo sheria ilikuwa inasema kwamba vyombo vya habari vitatoa taarifa kwa kuzingatia maslahi ya taifa, hivyo tunataka kama mwandishi amepata taarifa na akafanya ulinganifu wake vizuri basi tuache taarifa iandikwe,” amesema Wakili Marenga.

Aidha, Wakili Marenga amelitaja eneo jingine kuwa ni uundwaji wa Bodi ya Ithibati ambapo amesema chombo hicho kinateuliwa na Waziri wa Habari ambapo atahusisha Serikali na hivyo bado itakuwa na ukakasi.

“Kwa mujibu wa sheria hii chombo cha idhibati ndio kitakuwa na nguvu kubwa jambo ambalo hatuliungi mkono badala yake tunataka taaluma ya habari ijisimamie yenyewe kama ilivyo taaluma nyingine ikiwamo ya sheria,” amesema Wakili Marenga na kuongeza kuwa:
“Sheria pia imekuja na maeneo mawili ambayo imeyataja kama makosa ambayo ni uchochezi na kashifa, hili la kashfa sheria inaeneleza kuwa ukiandika jambo na likamfanya mtu adharaulike basi litakuwa ni kosa la jinai.

“Eneo hili ni changamoto kwa waandishi wa habari kwani mwandishi anaweza akawa anataka kuandika habari njema juu ya ubadhilifu au jambo lilote lakini mlalamikaji akikupeleka mahakamani basi linakuwa ni kosa la jinai, hili sisi tunapendekeza yawe madai na siyo jinai,” amesema Wakiliwa Marenga.

Wakili Marenga amesema kuwa katika eneo hilo la uchochezi sheria inasema kuwa jambo lolote litakaloandikwa na mwanandishi wa habari wananchi wakalisoma na wakaichukia serikali yao iliyoko madarakani basi atakuwa ni mchochezi ambapo anaweza kufungwa siyo chini ya miaka mitano jela.

“Hii inamaana kwamba unaweza hata kufungwa miaka 10, hivyo serikali imelipokea na imeahidi kulifanyia kazi.

“Kwani kwa kubaki hivyo ilikuwa inaondoa uhuru wa waandishi wa habari kufanya kazi za uchunguzi,” amesema Wakiliwa Marenga.
Amejata eneo jingine kuwa mamlaka ambayo ilikuwa ikipewa jeshi la polisi ya kwenda kwenye chombo cha habari na kukamata vifaa vya wanahabari bila idhini ya mahakama ambapo amebainisha kuwa serikali imepokea jambo hilo na kuahidi kulifanyia kazi.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile.

Itakumbukwa kuwa mapema mwezi huu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF), Deodatus Balile alisema kuwa yapo matumaini kwamba mapendekezo ya mabadiliko ya ya sheria yakasomwa kwa mara ya kwanza katika Bunge la Septemba, mwaka huu.

“Mchakato umeanza kuzaa matunda na katika bunge lijalo Septemba, mwaka huu tunaweza kuona hii sheria imepelekwa bungeni kwa ajaili ya kusomwa kwa mara ya kwanza,” alisema Balile.

Wadau wa habari nchini wanaendelea na kuhimiza serikali kufanya mabadiliko ya baadhi ya vifungu kwenye sheria ya habari ambavyo vimekuwa changamoto katika tasnia hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles