25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Bonnah azindua mkakati uhamasishaji sensa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, amezindua mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.

Mkakati huo umefanyika kupitia bonanza maalumu aliloliandaa ambalo limeshirikisha vikundi mbalimbali vya jogging na kufanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mwale iliyopo Kata ya Kiwalani.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, akizungumza wakati wa bonanza maalumu lililoandaliwa na Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, kwa lengo la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan na kuhamasisha wananchi kujiandikisha wakati wa sensa.

Bonanza hilo pia lilikuwa na lengo la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi anazozifanya kuleta maendeleo ya kiuchumi na kuhamasisha wananchi kuhesabiwa.

Akizungumza katika bonanza hilo Bonnah amesema sensa ina umuhimu mkubwa kwani inasaidia utekelezaji mipango ya bajeti na ugawaji wa rasilimali.

“Naomba tujitokeze kwa wingi kuhesabiwa ili mwaka ujao tuweze kupangiwa bajeti inayoendana na idadi ya watu ambao tuko Jimbo la Segerea, mkijiandikisha mtaiwezesha Serikali kupanga bajeti yake vizuri,” amesema Bonnah.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika bonanza hilo amewataka wananchi kuepuka upotoshwaji kuhusu zoezi hilo kwani lina nia njema ya kuiwezesha Serikali iweze kupanga mipango yake ya maendeleo.

“Hakuna Serikali inayoweza kuleta maendeleo kwa wananchi wake bila kufahamu idadi ya wananchi inaowahudumia, hatuwezi kujenga shule kama hatuna uhakika na idadi ya watu katika eneo husika.

“Tunatakiwa tujulikane idadi yetu ili mheshimiwa mbunge anavyopeleka maombi asitumie nguvu kubwa, atumie idadi ya wananchi anaowasimamia na kuwahudumia…mtaifanya kazi ya mheshimiwa mbunge kuwa nyepesi mtakapojitokeza kuhesabiwa,” amesema Ludigija.

Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza jamii kutowaficha watu wenye ulemavu kwani wana haki sawa kama wengine wasio na ulemavu.

Ludigija amempomngeza mbunge huyo kwa kuwaunganisha wananchi na kusimamia vema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

“Umekuwa ni mbunge wa mfano, ni mbunge ambaye hachoki, umekuwa kila wakati ukifuatilia miradi inayoendelea kwenye jimbo lako na mingine ilikuwa inaibuliwa unakwenda kuwatetea wana Segerea wapate fedha zaidi,” amesema Ludigija.

Katika bonanza hilo Bonnah ameahidi kutoa pikipiki mbili na viti 100 kwa klabu ya jogging ya AR NABU kuiwezesha kujiendeleza zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles