Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na wadau mbalimbali wameadhimisha siku ya wakulima wa shayiri mwaka 2022, na kujidhatiti kuboresha mnyororo wa thamani kwa kuwawezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa ili kuongeza tija.
Siku ya wakulima ya mwaka huu inayobeba kauli mbiu ya “kilimo cha kisasa, kuboresha mnyororo wa thamani”, imeangukia msimu wa mavuno wa shayiri, moja ya mazao muhimu ambayo TBL inanunua kwa wakulima.
Siku hiyo iliadhimishwa Monduli Juu, mkoani Arusha na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe kama mgeni rasmi.
Pia maadhimisho hayo yaliudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wakulima wa shayiri, wawakilishi wa TBL, mashirika ya kifedha, makampuni ya bima, maafisa ugavi na wanasayansi walioshirikishwa kwenye kuunda mbinu za kilimo na mbegu mpya.
Mtaalamu wa Kilimo wa TBL, Joel Msechu alisema, “TBL tunaamini kwenye nguvu ya kujenga ushirikiano na kwa maendeleo endelevu. Maadhimisho haya ya siku ya wakulima ambayo tumekuwa tunayaandaa kila mwaka kwa miaka mingi sasa, yanatoa nafasi kwa wakulima wa shayiri na mtama, tunaamini kuwa mjumuiko huu utawapa ujuzi wa kutatua changamoto wanazozipitia mashambani,” amesema Msechu.
Aidha, Msechu ameongeza kuwa, TBL imejidhatiti kuwawezesha wakulima kwa kuwapatia masoko ya uhakika ya mazao yao na vile vile kuwapatia ujuzi utaowawezesha kufanya kilimo cha kisasa na endelevu kitakachowawezesha kukua zaidi na hatimaye kuongeza mchango wa sekta ya kilimo kwenye uchumi wa taifa kama ilivyoidhinishwa kwenye kampeni ya kilimo ya Ajenda 10/30 ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kuwawezesha wakulima wadogo ni moja ya ahadi za AB InBev kama sehemu ya kutimiza malengo endelevu mwaka 2025, ambayo yanaafikiana na malengo endelevu mwaka 2025 ya umoja wa mataifa (SDG),” amesema Msechu.
Miaka ya nyuma, maadhimisho ya TBL ya siku ya wakulima yamedhihirisha kutoa nafasi kubwa ya kushirikishana ujuzi wa kilimo ili kukuza uzalishaji wenye tija, na vile vile kuwapa wakulima nafasi ya kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo.
Pia, wakulima wanapatiwa mrejesho juu ya msimu ulipita na kupata nafasi ya kujifunza njia fanisi za kilimo kupitia mashamba ya mfano. TBL hutumia nafasi hii kuonyesha utayari wake wa kufanya kazi moja kwa moja na wakulima wadogo na kuwapatia masoko ya uhakika ya mazao yao.
Mwaka jana, maadhimisho ya siku ya wakulima yalijikita kwa wakulima wa zabibu na kuainisha mafanikio makubwa kwa wakulima wa zabibu na kuingizwa rasmi kwenye kilimo cha kimkataba na TBL kwa lengo la kukuza kilimo cha zao la zabibu ili kuchangia uzalishaji endelevu wa zabibu nchini.