NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mholanzi Hans van Der Pluijm amesema hawezi kumlaumu yeyote kwa matokeo ya sare ya bao 2-2 waliyoyapata juzi dhidi ya wapinzani wao Azam FC, mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga hadi sasa imejikusanyia pointi 47 katika msimamo wa ligi sawa na wapinzani hao Azam FC wanaoshika nafasi ya pili wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Pluijm alisema siku zote mpira hautabiriki lolote linaweza kutokea tofauti na jinsi unavyopanga, hivyo haoni sababu ya kumlaumu mchezaji wala mwamuzi kwa kilichotokea uwanjani.
“Tuliingia uwanjani kwa nia ya kushinda na hata wapinzani wetu nao walikuwa na lengo hilo la kupata ushindi, lakini matokeo yamemalizika kwa sare ya 2-2 si mazuri ingawa naona yatakuwa yamewapa furaha sana Azam, kwani wametubania ushindi ila ndio mchezo.
“Lakini nawashangaa kwanini wanamlaumu mwamuzi kwa kutokuwapa penalti ambayo wanadai waliipata, kwani hata kama ikiwekwa CD ya mchezo huu kwenye TV sasa hivi mtaona haikustahili kuwa penalti, kwani Donald Ngoma alisukumwa akaanguka na mpira ukamjia mikononi akiwa kwenye 18 hivyo mwamuzi alikuwa sahihi,” alisema.
Alisema kwa ujumla mchezo ulikuwa wa kawaida sana, wachezaji wake waliweza kujitahidi kuwadhibiti Azam ingawa kipindi cha pili waliweza kusawazisha kwa bao rahisi.
Alieleza sare hiyo haiwanyimi kufanya vizuri kwenye mchezo wao wa kimataifa wa ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR ya Rwanda, unaotarajiwa kupigwa Machi 12 nchini humo, kwani mpango wao wa kupata ushindi uko pale pale.
Wakati huo huo katika hali isiyotegemewa, kocha Pluijm almanusura asusie mkutano na waandishi wa habari uliofanyika baada ya mchezo huo akihoji kwanini Azam wamlete kocha msaidizi Denis Kitambi kuzungumzia mchezo wakati kocha mkuu Stewart Hall alikuwepo uwanjani.
Lakini Mkuu wa Idara ya Habari ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, alijitahidi kumuelewesha ndipo alipoamua kuzungumza huku akionyeshwa kabisa kutoridhika na kitendo hicho.