WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemlilia aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, marehemu Trasias Kagenzi na kusema kuwa Taifa limepoteza mtumishi makini.
Akizungumza na wananchi waliofika nyumbani kwa marehemu eneo la Uzunguni mjini Maswa jana, Majaliwa alisema amepokea kwa mshutuko mkubwa kifo hicho.
marehemu Kagenzi alifariki dunia juzi, baada ya kusumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.
Alisema enzi ya uhai wake Kagenzi alikuwa mchapa kazi na mwadilifu na kuwa Taifa limepoteza mtumishi aliyekuwa akiendana na kasi ya Rais Dk. John Magufuli.
Alisema akiwa katika ziara ya siku ya nne mkoani Simiyu, alipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo, Ellaston Mbwilo ambaye alimjulisha juu ya kifo hicho.
Alisema muda mfupi kabla ya kupatwa na mauti, marehemu Kagenzi alikuwa akiendelea kuchapa kazi ofisini kwake..
Marehemu Kagenzi alizaliwa Kijiji cha Nyandutu wilayani Karagwe mkoani Kagera, Oktoba 21,1960.
Mwili wa marehemu Kagenzi, unatarajiwa kusafirishwa leo kwenda kijijini
kwao Nyandutu kwa mazishi na msafara huo utaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Ellaston Mbwilo.