WELLINGTON, NEW ZEALAND
ALIYEKUWA nyota wa mchezo wa kriketi nchini New Zealand, Martin Crowe, amefariki dunia juzi kutokana na ugonjwa wa kansa.
Mchezaji huyo alianza kugundulika kuwa na ugonjwa huo tangu mwaka 2012 na kuamua kutangaza kustaafu mchezo huo ambao ulimpa jina kubwa duniani.
Crowe amepoteza maisha huku akiwa na umri wa miaka 53 na kuacha mke Lorraine Downes pamoja na watoto watatu Emma, Hilton na Jasmine.
Familia ya marehemu ilisema kwamba, mchezaji huyo alikutwa na umauti huku akiwa amezungukwa na familia yake pamoja na marafiki kwenye hospitali iliopo mjini Wellinhton nchini humo.
Ilidaiwa kwamba hatua ya ugonjwa ambayo alifikia mchezaji huyo alikuwa hawezi kuishi ndani ya miezi 12 ijayo kwa kuwa hali yake ilizidi kuwa mbaya tofauti na awali.
Crowe aliisaidia timu yake ya Taifa ya New Zealand kutwaa mataji mbalimbali huku akichukua ubingwa mara tatu wa dunia akiwa na timu hiyo.