Na Denis Sikonde, Songwe
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ileje mkoani Songwe imefanikiwa kuzitembelea familia zilizopoteza ndugu Watano wa familia mbili tofauti aliwepo Mama mjamzoto wa mimba ya miezi tisa katika kata ya Sange na Ngulugulu wilayani humo.
Akizungumza kwaniaba ya Kamati hiyo, Hebroni Kibona amesema kama chama wamefika kwa ndugu hao lengo likiwa ni kiwafariji na kuwapa mkono wa pole, baada ya kupoteza ndugu zao.
Kibona amesema kamati ya siasa imefanikiwa kuchangishana fedha Sh 200,000 ambapo kwa kila familia wametoa Sh 100,000.
“Kama chama bado kinaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu kwao kwa kupoteza ndugu zao ambao walipoteza maisha baada ya nyumba zao kubomoka kwa kuangukiwa na magema ya milima katika Kijiji cha Sange kata ya Sange na kijiji cha Kisyesye kata ya Ngulugulu,” amesema Kibona.
Kibona amesema waliofariki dunia katika tukio la Kijiji cha Sange ni mke na mume pamoja na mtoto(4) huku mwanamke huyo akiwa na mimba ya miezi 9, ambapo kwa kata ya Ngulugulu Kijiji cha Kisyesye wanafamilia wawili walifariki dunia.
Katibu wa CCM wilayani humo, Hassan Lyamba amesema kamati ya siasa imeungana na famalia hizo katika kipindi hiki kigumu cha kupotelewa na ndugu zao, katika tukio lililotokea Aprili 28, 2022, ambapo chama na serikali wapo sambamba na familia zao.
Aidha, amewasihi kwamba katika kipindi cha msimu wa mvua wananchi kuchukua tahadhari ya mapema hususan Tarafa ya Bundali ambapo udongo ni tifutifu na kusababisha magema kupolomoka hivyo kuweka maisha ya wananchi hatarini.
Diwani wa Kata ya Ngulugulu, Joshua Swila akizungumza baada ya kupokea salamu hizo kwaniamba ya familia hizo ameipongeza kamati ya siasa kwa kuamua kutembelea familia zilizopoteza ndugu zao na kuipongeza serikali kuwa na jitihada za kufungua barabara.