Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Ukipita katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Kipunguni hivi sasa si rahisi kuona takataka zikiwa zimezagaa kama ilivyokuwa hapo awali.
Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni kimechangia kufanikisha hali hiyo kutokana na kuzigeuza taka kuwa mkaa na hivyo kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaochangiwa na ongezeko kubwa la taka na uchafu wa majumbani.
Ujuzi huo wa kutengeneza mkaa mbadala waliupata kupitia mradi wa ‘Taka ni Mali’ unaotekelezwa na Shirika la Amref Health Africa ambalo limekuwa likitoa mafunzo kwa vikundi mbalimbali vya kijamii vikiwemo vituo vya taarifa na maarifa ambavyo viko chini ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kikiwemo Sauti ya Jamii Kipunguni.
Mradi huo unahusisha pia kufungwa kwa mashine mbalimbali za kuchakata mkaa, tanuri la kuchakata taka na gari la kubebea taka.
Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Selemani Bishagazi, anasema malighafi za kutengeneza mkaa huo ni taka zinazozalishwa majumbani yakiwemo mabaki ya chakula, chenga za mkaa, mabaki ya mbao zilizoparazwa na nyingine.
Anasema taka hukusanywa na kuwekwa kwenye tanuri na kuchomwa kitaalamu kwa saa kadhaa kisha hugeuka kuwa majivu meusi ambayo huchanganywa na uji wa muhogo na kuyafanya kushikana tayari kwa kuingizwa kwenye mashine ili kuweka muonekano na kushikamana vema.
“Wateja wetu wakubwa ni wanajamii na kilo moja ya mkaa wa kawaida inauzwa Sh 2,000 lakini huu wa kwetu ni Sh 500 ambao unaweza kupika mahitaji yako yote kwa siku,” anasema Bishagazi.
Kikundi hicho hivi sasa kinamiliki kiwanda cha mkaa mbadala ambacho kwa kuanzia kimetoa ajira kwa watu 30 wakiwemo vijana waliokuwa wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu na waliokuwa wakitumia dawa za kulevya.
Bishagazi anasema kiwanda hicho kitazalisha tani mbili kwa siku na wanatarajia kuendeleza teknolojia hiyo kwa wanavikundi wengine kwani mkaa huo ni rafiki wa mazingira.
“Mipango yetu ni kuendelea kuboresha mazingira ili kupunguza uwezekano wa mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu na mengine lakini pia tunyanyuane kiuchumi, kwa sababu teknolojia hii ikisambazwa watu wengi watapata ajira na kwa watumiaji wataokoa fedha nyingi ambazo watazielekeza katika matumizi mengine kwa sababu mkaa huu unauzwa kwa bei nafuu,” anasema.
Mmoja wa wananchi wa Kipunguni, Queen Steven, anasema ameondokana na matumizi ya kuni na mkaa na kuanza kutumia mkaa huo ambao ni rafiki kwa mazingira na wenye gharama nafuu.
“Mkaa huu unanisaidia kwa sababu niliokuwa napata kwa Sh 2,000 kwa sasa napata kwa Sh 500 na fedha inayobaki inanisaidia kwenye mahitaji mengine kama kuongeza kwenye mboga au kuweka akiba. Pia tulikuwa tunalipa ada ya taka Sh 5,000 lakini sasa hivi wanakuja Sauti ya Jamii Kipunguni kuja kubeba taka,” anasema Queen.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Daniel Malagashimba, anakiri kuwa mradi huo umeleta manufaa makubwa kwa kutoa ajira kwa vijana, kupunguza uhalifu na kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
“Najivunia Mtaa wa Amani kuwa na fursa hii kwa sababu jamii imeelimika inatambua taka ni malighafi na mazingira yanakuwa masafi. Unanisaidia katika ulinzi na usalama tumekuwa hatutumii nguvu kubwa…vijana ukiwatengenezea fursa hata ukabaji wanaacha kwa sababu wanakuwa na uhakika wa kipato,” anasema Malagashimba.
Mwanakikundi mwingine wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Tausi Hassani, analishukuru shirika la Amref kwa kuwapatia mafunzo na mashine ya uzalishaji mkaa huo ambayo imesaidia kutunza mazingira na kutoa ajira kwa vijana na kuliomba liendelee kuwezesha jamii nyingine.
HALI ILIVYO
Kila mwaka takribani hekta milioni moja za miti ambazo ni asilimia 70 zinakatwa kwa ajili ya mkaa na kutokana na hilo asilimia 61 nchi inakabiliwa na jangwa.
Takwimu za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zinaonyesha mahitaji ya nishati ya mkaa nchini yanafikia tani milioni mbili hadi tatu kwa mwaka na ili kuzalisha tani moja ya mkaa zinahitajika mita za ujazo 10 hadi 12 za miti.
Kulingana na utafiti wa TFS, Dar es Salaam pekee huingizwa magunia zaidi ya 500,000 ya mkaa kila mwezi.