25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Vijana washauriwa kutumia mitandao ya kijamii kujikwamua kiuchumi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Vijana nchini wameshauriwa kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ili iweze kuwakwamua kiuchumi badala ya kujadili mambo ambayo hayana tija kwa ustawi wao.

Baadhi ya vijana walio katika majukwaa wakijadili maendeleo yao na shughuli za kukuza uchumi katika kongamano lililoandaliwa na CAFLO.

Akizungumza wakati wa kongamano la vijana walio katika majukwaa lililoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la CAFLO, Mtendaji wa Mtaa wa Mtambani uliopo Kata ya Vingunguti, William Kibeyo, amesema mitandao ya kijamii inatumiwa na watu wengi hasa vijana hivyo ikitumika ipasavyo itasaidia kuwakwamua kiuchumi.

“Vijana wengi bado hawajatambua faida za kutumia mitandao ya kijamii ili kupata fursa mbalimbali katika maisha, huwezi kufanikiwa kama umelala ndani unacheza na simu…mitandao ya kijamii itumike kuwaendeleza na si vinginevyo,” amesema Kibeyo.

Mtendaji huyo pia amewapongeza vijana wanaojihusisha na uuzaji vitafunwa (Chipp Chapp Group) kutoka Vingunguti ambao walipata mafunzo ya ujasiriamali kutoka Caflo na kukiri kuwa yeye na baadhi ya watendaji wengine ni wateja wa bidhaa zinazozalishwa na kikundi hicho.

Jackline Nkossa kutoka katika kikundi hicho amesema mitandao ya kijamii imewawezesha kupata wigo mpana wa wateja hatua iliyowawezesha kufungua ofisi nyingine.

“Tumekuwa tukijitangaza kwenye Facebook, Instagram, Twitter na WhatsApp na hii imetusaidia kupata wateja wengi. Tuna ofisi Vingunguti na Kijitonyama na tuna mpango wa kufungua matawi mengine Tabata na Kiwalani…hata kama ukitupigia ukasema unahitaji ndizi moja ya Sh 300 au Chipsi za Sh 500 sisi tunakuletea,” amesema Jackline.

Hata hivyo baadhi ya vijana wametaja changamoto zinazokwamisha maendeleo ya majukwaa kuwa ni pamoja na vikundi kutosajiliwa kwa wakati, kukosa ushirikiano miongoni mwao, ubinafsi na kukosa uvumilivu.

Kwa upande wake Mratibu wa CAFLO, Emmanuel Ngazi, amesema; “Tunataka kila kijana awe mshiriki hai katika kukuza uchumi ndiyo maana tunajitahidi kuwafikia vijana kwa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali.

Miongoni mwa mada zilizojadiliwa kwenye kongamano hilo ni umuhimu wa vijana kuboresha bidhaa na kutafuta masoko endelevu, kutumia mitandao ya kijamii katika kutangaza bidhaa na kutafuta masoko endelevu, kurasimisha bidhaa na umuhimu wa kulipa kodi.

CAFLO limekuwa likiwajengea uwezo vijana kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali na kuwaelekeza namna ya kuunda majukwaa hatua iliyosaidia baadhi yao kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi mbalimbali huku wengine wakifaidika pia kwa kupata mikopo inayotolewa na halmashauri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles