Na Clara Matimo, Mwanza
ILI kuendana na mahitaji, mwamko mkubwa wa wananchi kupanda miti nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa maelekezo kwa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na Mfuko wa Misitu (TAWA) kuharakisha uanzishwaji wa bustani huku wakitakiwa kuanzisha bustani nyingine ndogo kuanzia ngazi ya kata na tarafa kisha kubaini, kutenga maeneo sahihi ya kupandwa miti pia kuainisha aina ya miti itakayofaa kulingana na eneo husika.
Maelekezo hayo yametolewa leo Machi 21, 2022 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Marry Masanja, katika kilele cha maadhimisho ya siku ya upandaji miti na misitu kitaifa yaliyofanyika uwanja wa Sabasaba wilayani Magu Mkoa wa Mwanza.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo,Dk. Damas Ndumbaro, mbele ya wananchi waliojitokeza kwenye maadhimisho hayo, Marry amesema wananchi wamekuwa na mwamko wa kupanda miti katika maeneo yao hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha miche bora inapatikana wakati wote kwa urahisi na kutoa elimu ya ugani kwa wananchi kuhusu upandaji miti.
“Ili kuwe na upatikanaji wa miti kwa wingi na kwa urahisi nawaelekeza TFS kwa kushirikiana na Tawa hakikisheni bustani mnayotaka kuianzisha inanza mara moja, miche ya aina zote kulingana na mahitaji ya wananchi ipatikane ikiwemo ya mbao, matunda, kivuli, mapambo, kuboresha ardhi na malisho ya mifugo,” amesema Marry na kuongeza:
“Pia anzisheni bustani nyingine ndogondogo katika ngazi ya kata na tarafa ili wananchi waishio vijijini waweze kuipata kwa urahisi, shirikianeni na ofisi za wakurugenzi wa halmashauri kufanya upembuzi yakinifu kubaini na kutenga maeneo sahihi pa kuanzisha bustani hizo, maeneo ya kupandwa miti na kuainisha aina ya miti itakayofaa kupandwa katika eneo husika ili kuwe na upandaji miti wenye tija.
“Ili tuwe na mipango halisia ya upandaji miti katika maeneo yetu ardhi na malisho ya mifugo ibainishwe kwa kufanya hivyo tutakuwa na makisio halisia ya mahitaji ya miche kwa msimu husika vingenevyo tutakuwa tukibahatisha tu, watendaji hususan wizara yetu toeni elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa upandaji miti na uhifadhi ili wajue na watambue faida za rasilimali misitu,” amesema.
Naibu huyo amesema katika maadhimisho hayo jumla ya miti 6,000 ilipandwa shule ya msingi Sagani wilayani Magu huku akiitaka halmashauri hiyo kuhakikisha miti iliyopandwa inatunzwa vyema kwa kuimwagilia maji ili ikue bila kubugudhiwa na mifugo pamoja na uchomaji moto ambapo miti itakayoshindwa kukua uwekwe utaratibu wa kurudishia mingine mapema.
Amesema Wilaya ya Magu ni miongoni mwa wilaya chache zinazonyemelewa na ukame hapa nchini pia zipo dalili za hatari ikiwemo ukosefu wa mvua za kutosha na zisizotabirika, kuanza kukauka kwa baadhi ya vyanzo vya maji hivyo serikali imeona maadhimisho hayo yatakuwa chachu kwa wananchi kupanda miti mingi zaidi katika maeneo wanayoishi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, amesema tangu Desemba 9 mwaka jana hadi Februari mwaka huu mkoa huo umepanda jumla ya miti 3,237,871 huku akiwataka wananchi, taasisi za serikali, binafsi na wadau wa misitu mkoani humo waendelee na juhudi za upandaji miti, uhifadhi wa misitu ili kuiwezesha jamii kunufaika na bidhaa pamoja na hudama za misitu endelevu.
Kamishna wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, amesema wamepokea maelekezo ya waziri huyo na watahakikisha wanayatekeleza kwa ufanisi huku akibainisha kwamba wameishaanza mkakati wa kuzijengea uwezo shule za msingi na sekondari ili zianzishe bustani zao na kuziendesha ili kuwa na misitu inayoweza kuzalisha mahitaji mbalimbali ya binadamu ikiwemo kuni na ikabaki bila kuathirika.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Mwanza, Antony Diallo, aliyewakilishwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho(UWT) mkoani humo, Ellen Bogohe, aliishauri serikali kurejesha utaratibu uliokuwepo miaka ya nyuma kila mwanafunzi kupanda mti na kuutunza hadi atakapohitimu ili kuendelea kutunza mazingira.
Mmoja wa wakazi wa wilaya ya Magu, Max Yombo, ambaye ana kitalu cha kuzalisha miche mbalimbali amemkabidhi waziri huyo miche 1000 ikiwemo ya matunda na mbao ili wizara hiyo iipande maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kutunza na kuhifadhi mazingira.
Maadhimisho ya siku ya misitu duniani yanatokana na Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwaka 2012 ambapo liliagiza nchi wanachama kuadhimisha siku ya misitu duniani Machi 21 kila mwaka malengo yakiwa ni kupaza sauti kwa ajili ya uhifadhi wa misituya aina zote na kuhifadhi mitiyote ambayo kwa namna moja au nyingine haipo maeneo ya hifadhi ya misitu kutokana na kutambua umuhimu wa misitu katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya watu ambapo kauli mbiu ni uhifadhi wa mazingira na matumnizi endelevu.
Tanzania imeadhimisha siku ya misitu duniani kwa mara ya kwanza mwaka huu huku maadhimisho hayo yakiongozwa na Kauli mbiu isemayo ‘mti wangu, taifa langu, mazingira yangu, kazi iendelee’.